Mtuhumiwa aibua utata kesi ya kina Mbowe

Mtuhumiwa aibua utata kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

  • Utata wa alipo mmoja wa watuhumiwa katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, uliibuka jana mahakamani baada ya shahidi kudai hajui kama mtu huyo yuko hai au ameshafariki dunia.


Dar es Salaam. Utata wa alipo mmoja wa watuhumiwa katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, uliibuka jana mahakamani baada ya shahidi kudai hajui kama mtu huyo yuko hai au ameshafariki dunia.

Mohamed Ling’wenya alidai kuwa wakati wakikamatwa walikuwa na mtuhumiwa huyo, Moses Lujenge ambaye pia alikuwa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kikosi cha makomandoo.

Ling’wenya alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mbowe na wenzake.

Kesi hiyo ndogo iliibuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga kupokelewa kama kielelezo maelezo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi, Adam Kasekwa wakidai aliteswa na kutishwa kabla na wakati akitoa maelezo hayo.

Wanadai pia maelezo hayo yalitolewa saa nne, nje ya muda unaoruhusiwa kisheria. Kasekwa anadaiwa kukiri kosa katika maelezo hayo na kuwataja washitakiwa wengine kuwa alishirikiana nao. Wiki iliyopita, shahidi wa kwanza katika kesi ya msingi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai aliieleza wakati waliwakamata watuhumiwa wawili huko Moshi, hawakumpata Lujenge, licha ya kumtafuta sehemu mbalimbali wakiwa na watuhumiwa wawili.

Jana, Ling’wenya alidai wakati wakitolewa Kituo cha Polisi Tazara kwenda Kituo cha Polisi Mbweni akiwa amefungwa kitambaa usoni, mmoja wa maaskari alimweleza “mwenzako Moses Lujenge wameshamtupa kwa sababu alijidai kuwakimbia.”

Alipohojiwa na wakili wa Mbowe, Peter Kibatala, shahidi huyo alidai kwa maelezo hayo alielewa Lujenge ameshauawa.

Alidai hajawahi kumsikia (Lujenge) akitajwa mahali popote na upande wa mashtaka kama ataunganishwa katika kesi hiyo, hivyo hana uhakika kama yuko hai au ameshafariki dunia, hivyo hawezi kueleza mahali alipo.

Mbali na Mbowe, Mohamed na Adamu, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Halfani Hassan.

Wote wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, wakidaiwa kuyatenda kwa nyakati tofauti Agosti, 2020.


Shahidi akiri kuwa komandoo

Ling’wenya, aliyekuwa mwalimu wa mazoezi ya mapigano (Martial Art), baada ya kutoa ushahidi alihojiwa na mawakili wawili waandamizi wa Serikali ambao ni Abdallah Chavula na Robert Kidando.

Sehemu ya mahojiano hayo kati ya shahidi huyo na mawakili wa Serikali yalikuwa kama ifuatavyo:

Chavula: Mohamed Ling’wenya ulikuwa komandoo?

Shahidi: Ni sahihi, ukomando upo kwenye damu.

Wakili: Ni sahihi, ukomando na uanajeshi haufutiki hadi unakufa?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Hata masharti ya kijeshi na kikomandoo bado yanakufunga? Ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Miiko ya kijeshi na kikomando bado unafungwa nayo? Mfano kuongea mambo yanayotendeka ndani ya jeshi?

Shahidi: Yapi? Wewe ndio umeyasema.

Wakili: Jeshini kule ulipofuzu mafunzo ya kikomando ulikula kiapo au hukula?

Shahidi: Nilikula kiapo.

Wakili: Huko jeshini ulikuwa unatumikia mambo gani? Mambo mangapi taja matano.

Shahidi: Kulinda amani ya nchini, kulinda vifaa vya jeshi kama silaha na magari ya vita na kupigana vita.

Wakili: Vita ya wapi?

Shahidi: Force keeping ya Congo DRC.

Wakili: Shahidi umeieleza mahakama, wewe ulikuwa mwalimu wa makomando wa JWTZ, ni sahihi ?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Nitakuwa sahihi nikisema umefuzu digrii sita za ‘Martial Arts’?

Shahidi: Si kweli, sijafuzu.

Wakili: Ulikuwa unawafunza nini?

Shahidi: Kombati, kareti, parachuti.

Wakili: Kwa hiyo wewe unafahamu kupigana kareti?

Shahidi: Nafahamu.

Wakili: Ulijifunza kupigana kareti kwa muda gani ndani ya jeshi ? Ukiwa JWTZ?

Shahidi: Miezi sita, kikosi cha 92 KJ.

Wakili: Ulifanya awamu ngapi za mafunzo ya kareti pale kikosi cha 92 KJ?

Shahidi: Moja tu na nyingine nilifanya sehemu nyingine.

Shahidi: Nilipata mafunzo mengine ya kick box yaliyotolewa na Ufaransa miezi mitatu, kozi nyingine ilikuwa ya kuzuia uharamia ambayo ilifanyika Navy, mapigano ya kwenye majumba kwa muda wa miezi mitatu.

Wakili: Hivi kwenye mapigano ya kwenye nyumba ulikuwa unapiga na nani?

Shahidi: Ni jinsi ya kuwatoa maadui katika majumba.

Wakili: Ni mapigano gani ulikuwa umejifunza katika kupigana katika majimbo?

Shahidi: Kutumia silaha ambayo ni SMG na kisu.

Wakili: Mimi naamini ulichukuliwa na kuwekwa Special Force pale kikosi cha 92KJ, kwa kuwa umeaminika? Ni kweli au sio kweli.

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Ili uwe mwalimu wa mafunzo pale kikosi cha 92 KJ, unatakiwa uwe na sifa gani?

Shahidi: Kwa sifa sijui, ila nilipomaliza mafunzo, wakubwa walikaa na kuchagua jina langu, sasa sijui walitumia vigezo gani.

Wakili: Pale kikosini umekuwa mwalimu kwa muda gani ?

Shahidi: Mwaka mmoja.