Mtwara kupata Sh193.5 bilioni za miradi ya maji

Waziri wa maji, Mhandisi Isack Kamwelwe akiangalia mchoro unaoonyesha sehemu zitakazopata maji baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa Mapili katika kata ya Nanguruwe wilayani Newala mkoani Mtwara ambapo utahudumia zaidi ya wakazi 23,000.Kushoto kwake ni mkuu wa wilaya hiyo,Aziza Mangosongo.Anayeonyeshea mchoro ni mhandisi wa halmashauri ya wilaya ,Nsajigwa SadickPicha na Haika Kimaro
Muktasari:
Fedha hizo ni sehemu ya dola za kimarekani 500 milioni ambazo zinatarajiwa kutolewa na Serikali ya India kwa ajili ya kutekeleza miradi 16 ya maji nchi nzima, ukiwemo mkoa huo.
Mtwara. Mkoa wa Mtwara unatarajia kupokea dola 87.41milioni za Marekani ambazo ni takribani Sh193.5 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.
Fedha hizo ni sehemu ya dola za kimarekani 500 milioni ambazo zinatarajiwa kutolewa na Serikali ya India kwa ajili ya kutekeleza miradi 16 ya maji nchi nzima, ukiwemo mkoa huo.
Hayo yameelezwa jana Januari 17, 2018 na Waziri wa Maji, Isack Kamwele wakati akizundua miradi mitatu ya maji katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Masasi na halmashauri ya mji Newala ambayo imegharimu Sh4.36 bilioni.
Katika miradi hiyo mitatu zaidi ya wananchi 42,000 watanufaika, huku wakilazimika kuchangia Sh 50 kwa ndoo ya lita 20 na wazee wasiokuwa na wasaidizi watapatiwa ndoo nne za lita 20 bure kwa siku badala ya kununua ndoo moja ya lita 20 kwa Sh1000.
“Serikali ya India imeahidi kutoa dola za 500 milioni za Marekani kutekeleza miradi ya maji nchini na kati ya fedha hizo dola 87 milioni nitazileta Mtwara kutatua kero ya maji,” amesema na kuongeza,
“Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuona kila mwananchi anapata maji kwa umbali usiozidi mita 400 kama sera ya maji na ilani ya chama inavyoelekeza.”
Waziri huyo amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuvilinda ili kuendelea kupata huduma hiyo na kuziagiza idara za maji kuongeza vichoteo ili wananchi wapate maji kwa haraka.
Wakati wa uzinduzi wa mradi wa Mapili halmashauri ya mji Newala utakaohudumia zaidi ya watu 23,000, mkuu wa wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo amesema baadhi ya ndoa zimekuwa na mikwaruzano inayosababishwa na tatizo la maji.
“Katika baadhi ya maeneo ambayo hayana maji wanawake wanafumaniwa lakini kwa sasa tatizo hili kwa kata ya Nanguruwe halitakuwepo tena,” amesema Mangosongo.
Baadhi ya wananchi katika maeneo hayo wameishukuru Serikali kwa kuwaondolea kero iliyowakabili kwa miaka mingi na kuomba huduma hiyo isogezwe zaidi kwa wananchi.