Muhimbili yawasha mashine saba za watoto kusikia
Mtoto akishtuka baada ya kusikia sauti kwa mara ya kwanza. Jumla ya watoto saba leo wamewashiwa rasmi vifaa vya usikivu baada ya upasuaji wa kupandikizwa vifaa hivyo uliofanyika Juni mwaka huu.
Muktasari:
- Watoto saba waliopandikizwa vifaa vya kusikia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamewashwa mashine hizo, hatua inayowawezesha kuanza kusikia lugha na sauti kwa mara ya kwanza tangu walipozaliwa.
Dar es Salaam. Watoto saba waliopandikizwa vifaa vya kusaidia usikivu (Cochlear implant) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamewashiwa mashine hizo, hatua inayowawezesha kuanza kusikia lugha na sauti kwa mara ya kwanza tangu walipozaliwa.
Mashine 13 zimewashwa kwa watoto hao saba, kutokana na baadhi yao kuwekewa kifaa katika kila sikio. Tukio hilo limeelezwa kuwa mwanzo wa maisha mapya kwa watoto hao, ambao sasa wataanza kupokea mawimbi ya sauti kwa kiwango cha chini na kuzoeshwa taratibu hadi watakapoweza kusikia vizuri zaidi.
Akizungumza katika tukio hilo leo Jumatatu, Julai 27, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia dawa na vifaatiba, Emanuel Tayari amesema watoto hao wamefanyiwa upasuaji na jopo la wataalamu wazawa, jambo linaloonesha hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika utoaji wa huduma za kibingwa.
Amesema takribani watoto watano kati ya 1,000 wanaozaliwa nchini hupata changamoto ya usikivu. Kwa wastani wa watoto milioni 2.2 wanaozaliwa kila mwaka, hali hiyo inatafsiriwa kuwa karibu watoto 12,000 huzaliwa na changamoto ya kusikia kila mwaka.
Tayari amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha watoto wenye changamoto hizo wanapata matibabu na huduma za utengamao, akibainisha kuwa zaidi ya watoto 115 tayari wamefanyiwa upasuaji wa kupandikizwa kifaa cha kusaidia usikivu hapa nchini.
Amesema mafanikio hayo hayajatokana na bahati, bali ni matokeo ya uamuzi ya Serikali kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya.
Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, matumizi ya afya yameongezeka kutoka Sh1.19 trilioni mwaka 2015/16 hadi Sh2.97 trilioni mwaka 2025/26, ongezeko la Sh1.78 trilioni.
Ameongeza maendeleo hayo yamechangiwa pia na Mpango wa Samia Suluhu Scholarship, ambapo wataalamu watano kutoka kitengo cha masikio wamepata nafasi ya mafunzo ya kibingwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Dk Delila Kimambo, amesema hospitali hiyo imekuwa ikitoa rufaa ya watoto kwenda India kwa ajili ya upasuaji huo, hali iliyokuwa ikiigharimu Serikali kiasi kikubwa cha fedha.
Amesema katika kipindi cha nyuma, watoto 120 walipelekwa India kwa matibabu hayo, huku takribani Sh6 bilioni zikitumika. Hata hivyo, baada ya MNH kuanza kutoa huduma hiyo hapa nchini, gharama zimepungua na wazazi hawalazimiki tena kusafiri nje ya nchi.
Kwa sasa, MNH hufanya takribani upasuaji 20 wa kupandikiza vifaa vya kusikia kwa mwaka, huku gharama ya matibabu kwa mgonjwa mmoja ikifikia karibu Sh45 milioni. Sehemu kubwa ya gharama hizo hubebwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine.
Dk Kimambo amesema watoto hao sasa wanafanyiwa ufuatiliaji wakiwa pamoja na wazazi wao, ambao wataanza kuwasiliana nao kwa lugha na sauti huku wataalamu wa lugha na usikivu wakiendelea kuwasaidia baada ya upasuaji.
Amesema hospitali bado inahitaji wataalamu zaidi wa lugha na usikivu, kwa kuwa huduma hiyo ni muhimu katika kumsaidia mtoto kujifunza kusikia na kuzungumza baada ya kupandikizwa kifaa.
Naye Mkuu wa kitengo cha masikio, pua na koo wa MNH, Dk Aslam Nkya amesema watoto waliowashiwa mashine wataanza kupokea mawimbi ya sauti ya chini, kisha yataongezwa taratibu kwa kipindi cha mwezi mmoja ili waweze kuzoea vifaa hivyo.
Amesema kuwapa watoto mawimbi makubwa ya sauti kwa ghafla kunaweza kuwafanya waichukie mashine, hivyo mchakato huo hufanyika kwa uangalifu na ufuatiliaji wa karibu wa wataalamu.
Mzazi wa mmoja wa watoto hao, Nyange Matayra, ameishukuru Serikali, uongozi wa MNH na wataalamu kwa kufanikisha upasuaji wa mtoto wake na kumwezesha kuanza safari mpya ya kusikia.
Dk Kimambo amesema hadi sasa madaktari wazawa 32 wameanzishiwa mafunzo ya upasuaji wa sikio ili baadaye huduma hiyo ianze kutolewa katika hospitali za kanda. Pia, Tanzania ina madaktari bingwa bobezi wanne wa upasuaji wa sikio, huku lengo likiwa kufikia sita.