Muuguzi afutwa kwenye kada ya uuguzi kwa rushwa ya Sh40,000
Muktasari:
Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limemfuta kwenye orodha ya wauguzi aliyekuwa muuguzi wa zahanati ya Boholoi ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, John Chuma kwa kutiwa hatiani kwa makosa matatu likiwemo la kuchukua rushwa ya Sh40,000 ili amzalishe Zuhura Shabani.
Dodoma. Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limemfuta kwenye orodha ya wauguzi aliyekuwa muuguzi wa zahanati ya Boholoi ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, John Chuma kwa kutiwa hatiani kwa makosa matatu likiwemo la kuchukua rushwa ya Sh40,000 ili amzalishe Zuhura Shabani.
Katika mashtaka ya msingi John alidaiwa kufanya kazi ya uuguzi kinyume cha maadili kwa kuacha kumhudumia mgonjwa aliyefika kupata huduma, kushindwa kusimamia kiwango cha taaluma ya uuguzi kwa weledi na kupokea rushwa ya Sh40,000 kutoka kwa mteja Ili kumpa huduma ya uzazi.
Baraza limefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza pande zote mbili na kubaini Chuma alitenda makosa hayo kinyume cha Sheria ya uuguzi na Ukunga na kuhatarisha usalama wa mama na mtoto wake.
Leo Januari 25, 2023 mbele ya wajumbe wa Baraza hilo lililoongozwa na Mwenyekiti wao, Profesa Lilian Mselle, mlalamikaji Zuhura Shabani amesema alifika kwenye Zahanati hiyo Julai 3, 2022 kwa ajili ya kujifungua ndipo alipomkuta muuguzi John Chuma.
Zuhura amesema kwakuwa alikuwa na hali mbaya alipanda moja kwa moja kwenye kitanda cha kujifungulia, lakini muuguzi huyo alimshusha na kumuuliza kama ana Sh40,000 ili aendelee kumpa huduma ya uzazi.
"Nikamwambia sina hela, akaniambia nishuke lakini nikalazimisha kupanda huku nikiwa nasikia kusukuma mtoto nikapanda kitandani na nikajifungua mwenyewe na muuguzi alipoona mtoto katoka akaja kunitenganisha na mtoto huku akinibana na mikasi Ili itolewe hela ndipo aendelee na huduma nyingine," ameeleza Zuhura.
Akiendelea kutoa maelezo hayo amesema muuguzi huyo aliondoka bila kumsafisha akidai apatiwe fedha ndipo atoe huduma hiyo hivyo mama mzazi wa Zuhura alimpa fedha alizotaka muuguzi huyo kwa kuazima kutoka kwa Mchungaji wa Kanisa la Free Pentecoste Church of Tanzania (FPCT), Paulo Sebastian na alipokabidhiwa fedha hizo alirudi kumuhudumia.
Hata hivyo, baada ya Zuhura kutoa maelezo yake mshtakiwa Chuma alitakiwa kumuuliza maswali mlalamikaji na mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo;
Muuguzi: Zuhura ulipokuja kujifungua kituoni ilikuwa saa ngapi?
Mzazi: Ilikuwa saa tisa.
Muuguzi: Je, ulikuja na vifaa?
Mzazi: Ndio nilikuja na vifaa.
Muuguzi: Muongo, wakati na kukagua hukuwa na vifaa.
Mzazi: Nilikuwa na vifaa vyangu vyote.
Muuguzi: Hukuwa na ndoo, mipira, glovu na sio mimi niliyekwenda kukuchemshia maji kwa mke wangu, kataa.
Mzazi: Hapana hivyo vifaa alikuja navyo mama yangu vyote.
Muuguzi: Sijakuzalisha vizuri kweli?
Mzazi: Ulikataa.
Muuguzi: sikukutoa kondo la nyuma?
Mzazi: Ulitoa baada ya kupewa hela.
Muuguzi: Wakati DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) anakuja alikukuta kwenye hali gani na mtoto alikuwa kwenye hali gani?
Mzazi: Alimkuta mtoto amefungwa kitovu kwa kitambaa badala ya kifaa chake kwa kuwa ulikataa.
Baada ya Chuma kumuuliza Zuhura maswali mlalamikaji alikuwa na mashahidi wawili akiwemo Mchungaji Paulo Sebastian aliyemuazima mama wa Zuhura fedha za kumpa muuguzi na Yunus Salim mjumbe wa Kamati ya Zahanati hiyo.
Hata hivyo, baada ya kutoa hukumu hiyo Mwenyekiti wa Baraza hilo Profesa Lilian Mselle amemtaarifu John Chuma kuwa ana haki ya kukata rufaa ndani ya miezi mitatu kwa Waziri Afya ikiwa hajaridhika na maamuzi hayo.