Muuza mkaa ambwaga Naibu Spika

Muuza mkaa ambwaga Naibu Spika

Muktasari:

  • Mgombea Ubunge wa jimbo la Kuresoi Kaskazini, Alfred Mutai, ametangazwa kuwa mshindi wa jimbo hilo, akimbwaga Moses Cheboi ambaye ni Naibu Spika.

Nairobi. Mgombea Ubunge wa jimbo la Kuresoi Kaskazini, Alfred Mutai, ametangazwa kuwa mshindi wa jimbo hilo, akimbwaga Moses Cheboi ambaye ni Naibu Spika wa Bunge.

Kabla ya kuwania nafasi hiyo, Mutai alikuwa diwani wa Sirikwa kuanzia 2017, mwaka ambao aliingia kwenye medani za siasa, akitokea katika shughuli za uuzaji wa mkaa.

Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Lilian Akoth leo Alhamisi Agosti 11, 2022 amemtangaza Mutai kuwa mbunge kwa kupata kura 25,365 dhidi ya Cheboi ambaye amepata kura 20,395, Joel Ayeni amepata kura 2,435 na Joyce Chepkemoi amepata kura 567.

Mutai alikuwa akigombea kwa tiketi ya UDA alikuwa na mchuano mkali na Cheboi- aliyewania kinya’nganyi’ro kama mgombea huru.

Akizungumza na baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi katika kituo cha majumuisho ya kura cha sekondari ya Mau, Mutai aliwashukuru wote kwa kumpigia kura.

Mutai aliwaahidi kutanguliza masilahi yao mbele, akisema elimu, barabara na gharama nafuu za maisha ni miongoni mwa vipaumbele vyake, atakapoingia ofisini.

"Sio kazi rahisi ni safari ndefu tangu tunaanza kupiga kura ya kusaka ushindi.Ushindani ulikuwa mgumu, lakini tulifanya vizuri katika kampeni zetu,” amesema Mutai.