Mvua kubwa yabomoa nyumba 10 Morogoro

Diwani wa kata Mkundi Manispaa ya Morogoro, Seif Chomoka na Diwani Viti Maalumu CCM, Grace Mkumbae wakitoka kukagua nyumba ya mmoja wa wakazi wa mtaa wa Mawasiliano inayotishiwa kumegwa na maji ya mvua kutokana na korongo la Mgulu wa Ndege mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika Manispaa ya Morogoro imesababisha nyumba zaidi ya 10 kubomoka katika kata ya Lukobe na Mkundi katika Wilaya ya Morogoro.

Morogoro. Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika Manispaa ya Morogoro imesababisha nyumba zaidi ya 10 kubomoka katika kata ya Lukobe na Mkundi katika Wilaya ya Morogoro.

Mvua hiyo ambayo imeanza usiku wa kuamkia leo Jumatano Februari 2, 2022 imesababia mafuriko ambayo pia yamesomba mali na kuharibu vitu mbalimbali.

Mafuriko hayo yalitokea maeneo ya Juhudi, Tushikamane, Cap town, Manyuki, Mjimpya, Azimio na Kwawagogo.

Akizungumza na Mwananchi leo mwenyekiti wa mtaa wa Tushikamane, Omary Hassan amesema kuwa baada ya tathimini ya athari za mafuriko wamebaini kuwa nyumba zilizingirwa na maji lakini walifanikiwa kuwaoko watu waliokuwa kwenye nyumba hzio.

Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Kilongo B kata ya Mkundi, Paul Madova amesema nyumba zaidi ya 20 zimeingia maji katika mtaa huo.

Mwanafunzi wa shule ya msingi Lukobe, Happyness Manga (13) amesema mvua hiyo imeharibu vifaa vyake vya shule na leo hajaweza kwenda shule huku mtaa huo ukiathirika zaidi kwa nyumba kuingia maji.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Goodluck Zelote amesema kuwa walianza kuokoa watu na mali kanzia jana Jumanne usiku mpaka leo.

Zelote amesema kuwa bado hakuna taarifa za vifo wala majeruhi.