Mvua ya dakika 45 yakata mawasiliano barabara ya Buchosa na Sengerema

New Content Item (2)

Baadhi ya abilia walipokuwa wakisafiri kutoka Buchosa kwenda Sengerema wakishuhudi maji yaliyokata barabara kwenye Kijiji cha Mizorozo  Kata ya Kalebezo hali iyosababisha magari kushindwa kupita na kukwamisha magari kuvuka. Picha na Daniel Makaka

Muktasari:

  • Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza zimeleta adhari za kukatika kwa barabara inayounganisha Sengerema na wilaya Buchosa na kuleta adha kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Buchosa. Mvua iliyonyesha takribani dakika 45 jioni leo Desemba 7, 2023 kwenye Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza imekatisha mawasiliano kati ya Sengerema na Buchosa baada ya kukatika kwa barabara kwenye Kijiji cha Mizorozo kata ya Kalebozo na kuleta adha Kwa watumiaji.

Tukio hili ni la pili kutokea  mwaka huu ambapo Novemba 27,2023 mvua iliyonyesha takiriba saa saba ilikatisha  mawasiliano ya barabara hiyo yenye kiwango cha vumbi kwenye kijiji Cha Luchili na kitongiji cha Iseni  ambapo abiria walikwama kwa saa kadhaa kutokana na kukatika kwa barabara hiyo.

Akizungumuza na Mwananchi kwa njia usiku huu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa, Idama Kibanzi amesema baadhi ya abiria na magari yamekwama kutokana na kukatika mawasiliano hivyo wanaziomba mamulaka husika kuchukuwa jitihada za mapema  ili kukabiliana na hali hiyo.

Amesema wananchi wameanza kuhoji huku wakimtupia lawama  mkandarasi aliyepewa zabuni ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami amechelewa kuanza ujenzi huo na kuzua maswali mengi yasiyo na majibu.

"Serikali inatakiwa kuingilia kata suala hili ili mkandarasi aanze kazi ,suluhisho la barabara hii kuwa bora ni kujengwa kwa kiwango cha lami ,amesema Idama.

Mkazi wa Kijiji cha Kalebezo Ahamed Yusuphu aliyefika eneo la tukio na  kushuhudia tukio hilo amesema magari yamekuwa yakifaulisha abilia kutokana na kushindwa  kupita hivyo jitihada za haraka zinatakiwa ili kuwanusuri watumiaji wa barabara hiyo.

Taarifa zilizoifikia Mwananchi usiku huu zinasema tayari ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo imefika eneo la tukio na kujione  hali hiyo.
Katibu wa mbunge huyo Julias Butongwa amesema tayari wamewasiliana na  wakala wa barabara mkoa wa Mwanza kufika na kutoa huduma ya dharura ili wananchi waweze kupata huduma.

"Usiku huu wakala wa barabara mkoa wa Mwanza watafika eneo ambalo barabara imekataka na wataweanza matengenzeo ya kuweka makalavati kufika kesho asubuhi barabara itakuwa imeanza kupitika” amesema Butogwa.