Mvua yabomoa makazi Tegeta Nyuki, Mbezi Beach

Muktasari:

  • Mvua kubwa iliyoambatana na upepo inayoendelea kunyesha imeharibu makazi ya watu na miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam. 

Dar es Salaam. Wakazi wa Tegeta Nyuki na Mbezi Beach jijini hapa wamesema wako katika hali mbaya baada ya maji  ya mvua inayoendelea kunyesha leo Januari 20, 2024, kutuama na kubomoa makazi yao.


Mwananchi Digital, leo imefika Mbezi Beach na Tegeta Nyuki kushuhudia wingi wa maji hayo, huku wananchi wakieleza kilio chao. 


Kwa wakazi wa Mbezi Beach wakiwamo wafanyabiashara wa matofali wamesema matofali zaidi ya 300 yamesombwa na maji na mengine kuvunjika. 


Godfrey John mkazi wa Mbezi Darajani ambaye anafanya kazi kwenye mashine ya kufyatua matofali amesema mbali na matofali mashine nne za kufyatua matofali zimeharibika.


“Zaidi ya matofali 300 zimechukuliwa na maji na kuna nyumba jirani hapa imevunjwa na maji uharibifu ni mkubwa," amesema.


Aron Daudi, mkazi wa Tegeta Nyuki amesema eneo lenye baa, nyumba za kulala wageni zote zimesombwa na maji.


"Mbali na uharibifu kuna watu wamesomwa na maji mama, baba mwenye nyumba na mtoto ambaye ameokolewa," amesema Daudi.


Picha za video zilizosambaa mitandaoni zimeonyesha maji yakiwa yamejaa maeneo ya Mbweni JKT na kusababisha barabara kufungwa. 

Endelea kusoma tovuti yetu kwa taarifa zaidi