Mvua yabomoa nyumba tatu Lindi

Moja kati ya nyumba tatu zilizobomoka katika kijiji cha Mnyangala
Muktasari:
- Nyumba tatu zimebomoka kutokana na mvua kubwa kunyesha na nyingine 20 kuingia maji, huku zikiharibu mashamba kijiji cha Mnyangara.
Lindi. Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini zimebomoa nyumba tatu katika kijiji cha Mnyangara, kilichopo manispaa ya Lindi na nyingine 20 zikijaa maji, kutokana na kufurika kwa Mto Namilapo.
Akizungumza na Mwananchi leo Februari mosi, 2024, mwenyekiti wa kijiji hicho, Ally Kayoyo amekiri kutokea kwa matukio hayo ya nyumba kuingia maji na nyingine kubomoka pamoja na mashamba ya mpunga na mahindi kusombwa na maji.
“Karibu wananchi wote mashamba yao yameathirika kutokana na kujaa maji kwa mto Mbwemkuru na Mto Namilapo na kukasababisha maji kuingia kwenye nyumba 20 na tatu kubomoka. Tunachoshukuru hakuna madhara kwa binadamu, kwa wale ambao nyumba zao zimebomoka wameomba hifadhi kwa ndugu na wapo huko kwa sasa,” amesema Kayoyo.
Kayoyo amesema mvua zilizosababisha mashamba kujaa maji zilinyesha Januari 15, 2024 na hawajafanya tathmini kujua imesababisha hasara ni kiasi gani, wanasubiri hadi atakapofika ofisa kilimo.

Nyumba ikiwa imezingirwa na maji baada ya mvua kunyesha
“Tumetoa tahadhari kwa waliopo mabondeni na wanaoishi karibu na mto waondoke kwa sababu mvua zinaendelea kunyesha japo Mto Namilapo hautiririshi maji, muda wote unaweza ukapitisha maji saa mbili au tatu yakaisha,” amesema Kayoyo.
Sharifa Mfaume, mkazi wa kijijini hapo amesema mvua ilianza kunyesha saa tano na nusu asubuhi ilipofika saa saba mchana maji yakaanza kuingia ndani na kusababisha magodoro na vitu vingine kulowa.
“Nyumba haijabomoka lakini magodoro na vitu vingine vya ndani vililowa pamoja na simu yangu kuchukuliwa na maji. Kwa kweli hali ni mbaya, shamba langu la mahindi na mpunga kama heka moja na nusu vyote vimechukuliwa na maji, tumebaki tunashangaa tu, hatuna kitu mashambani,” amesema Sharifa.
Saidi Lilanje ni miongoni wananchi ambao nyumba zao zimebomoka baada ya mvua kunyesha na maji kuingia ndani, alianza kuhamisha vitu na kwa sasa amepata hifadhi kwenye nyumba ya mama yake mkubwa ambaye anaishi shambani.
Naye Mussa Mkulile, mkazi wa kijijini hapo amesema mashamba yameathirika na maji na hawajui cha kufanya, kwa sababu tangu kuanza Januari hazizidi siku tano ambazo hazijanyesha mvua.