Mvua yaleta maafa Rombo, mmoja afariki
Muktasari:
- Mvua hizo zinazoendelea kunyesha wilayani Rombo zimelata maafa ikiwemo mtu mmoja kufariki dunia, huku baadhi ya nyumba zilizopo katika vitongoji vitatu katika Kata ya Mamsera vikiathiriwa na mvua hizo.
Rombo. Mtu mmoja anayetambulika kwa jina la Costastine Aniset shao (45), mkazi wa Kijiji cha Mamsera Juu, Kata ya Mamsera, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, amefariki duniani baada ya nyumba yake kuangukiwa na ngema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani hapa.
Pamoja na mvua hizo kusababisha maafa ya mtu mmoja katika kata hiyo, yapo maeneo mengine ambayo yameathiriwa na mvua hizo katika vitongoji vya Shao-Malamsha, Kilemeni na Kwa Mungu.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kusema wapo katika maeneo ambayo yameathiriwa na mvua hizo ili kujua ukubwa na athari zake.
"Ni kweli kuna tukio la mtu mmoja kufariki, na sasa hivi tupo kwenye haya maeneo ambayo yameathiriwa na mvua, tunazunguka kuangalia hali ilivyo," amesema Kanali Maiga.
Akizungumzia madhara ya mvua hizo, diwani wa kata hiyo, Sheldon Shayo amesema tukio la mtu huyo kufariki lilitokea usiku wa kuamkia Novemba 7 wakati marehemu akiwa amelala nyumbani kwake ambako anaishi mwenyewe.
"Juzi kulikuwa na mvua kubwa sana ambayo ilikuwa inanyesha, huyu baba wakati huo alikuwa amelala nyumbani kwake na anaishi mwenyewe baada ya kutengana na mke wake, mvua ilivyonyesha kubwa, ngema iliangukia nyumba yake na hivyo kufukiwa na udongo," amesema diwani Shao
Amesema athari hizo za mvua zimeleta hofu kubwa kwa wananchi wanaoishi katika kata hiyo hasa kwa wale wanaoishi maeneo ya milimani.
"Sasa hivi wananchi wameendelea kuingiwa na taharuki kubwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na wameiomba msaada wa kupata hifadhi mpaka mvua zitakapoacha kunyesha, hasa wananchi wanaoishi maeneo ya milimani," amesema diwani huyo.