Mwanafunzi kidato cha kwanza ajiua baada ya kuhojiwa na wazazi wake
Muktasari:
- Mtoto huyo amejiua baada ya wazazi kumhoji kuhusu tuhuma walizozipokea kutoka kwa majirani juu ya wizi wa fedha kwenye kibanda chao, kutohudhuria masomo shuleni.
Songwe. Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mpakani, Ufunuo Mwamlima (13), mkazi wa Tunduma mkoani Songwe, amejiua kwa kujichoma kisu tumboni baada ya wazazi wake kumhoji kuhusu mwenendo wa tabia zake zisizowaridhisha.
Mtoto huyo amechukua uamuzi huo baada ya wazazi kumhoji kuhusu tuhuma walizozipokea kutoka kwa majirani kuhusu wizi wa fedha kwenye kibanda chao pamoja na kutohudhuria masomo shuleni.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Fadhiri Mwamlima, baba mkubwa wa marehemu, amesema usiku wa Septemba 10, 2024 baada ya wazazi wake kumwita kijana wao kumhoji kuhusu wizi wa fedha kwenye kibanda cha jirani, kijana huyo alikiri.
Pia alisema ana chenji alizodai anaenda kuzichukua ili awaletee lakini baadaye walisikia kelele kutoka jikoni.
Mwamlima amesema mtoto huyo alikiri kuiba fedha zilizotokana na mauzo ya duka lililopo nyumbani baada ya kubaini kuporomoka kwa duka hilo ambapo alipoulizwa, kijana huyo kwa mara ya kwanza alikana na baadye kukubali kuwa huwa anaiba fedha kwa ajili ya kulia chakula shuleni.
“Baada ya kukiri kuiba fedha hizo, alisema chenji zipo chumbani, alipokuwa anakwenda chumbani, akaingia jikoni kuchukua kisu na kumuaga mdogo wake kwa kumpungia mkono na baadaye akajichoma na kisu tumboni,” amesema Mwamlima.
Amesema wazazi walipotoka walikuta kijana amejichoma kisu na utumbo uko nje na kuamua kumpeleka hospitali, lakini akafariki dunia wakiwa njiani.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Chapwa A, Steven Minga amesema alipokea taarifa kutoka kwa balozi wake na namna ulivyotokea licha ya jitihada za kuokoa uhai wa mtoto huyo, lakini umauti ulimkuta baada ya kufika hospitali.
Diwani wa kata ya Chapwa, Jackson Siame ametoa rai kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao ikiwepo kuzuia kuangalia filamu zenye maudhui ya kujiua ili kujiepusha na matukio ya mauaji kama yaliyomkuta kijana huyo.
“Tujaribu kuwaepusha vijana wetu kuangalia filamu hizi wanazoangalia, ukiangalia kijana huyu amefanya tukio hili kwa ujasiri, huenda imetokana na ujasiri wanaouangalia kwenye maudhui ya filamu hizo,” amesema Siame.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera amethibitisa kutokea kwa tukio hilo huku akishauri jamii ionapo mwananchi ana msongo wa mawazo, wajue namna ya kulitatua ili kuepusha vifo vya watu kujiua.