Mwanamke auawa na mamba akichota maji Ludewa

Mwanamke auawa na mamba akichota maji Ludewa

Muktasari:

Marehemu aling’atwa na mamba mkononi na kuzamishwa majini hali iliyomsababisha kupoteza maisha.

Ludewa. Mkazi wa Kijiji cha Kipingu, mkoani Njombe, Corester Haule (25) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mamba alipokuwa akiteka maji katika mto Ruhuhu.

 Akieleza tukio hilo jana Agosti 15, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Alphonce Mbeya amesema tukio lilitokea Agosti 13 majira ya saa 12 jioni wakati Corester na wenzake wakichota maji.

"Tukio lilitokea majira ya saa 12 jioni nikiwa eneo la pantone ambalo haliko mbali na mahali lilipotokea tukio, nikaja kuitwa na kujuzwa kuwa kuna mtu kakamatwa na mamba.

“Nilikimbia kufika pale ikanibidi niwaambie watu wachukuwe mitumbwi tukamuokoe marehemu. Tukaanza kumkimbiza mamba, hatimaye akauacha mwili wa marehem.

“Tukauchukua na kuulaza kwenye mtumbwi na kupeleka sehemu ya forodha. wakaja maaskari kuangalia mwili baadae wakaturuhusu turudi nao nyumbani," amesema Mbeya.

Amesema kuwa marehemu aling’atwa mkononi na kuzamishwa majini hali iliyosababisha kifo chake.

Mbeya ameiomba serikali kurekebisha mradi wao wa maji uliosimama kutokana kwa kukosekana umeme, hali inayo walazimu wananchi kufuata maji mtoni ambako ni hatari kwa maisha yao.

Mbunge wa jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga alifika kutoa salamu za pole na kumwomba Waziri wa Maliasili na Utalii kutoa kibali kwa wananchi kuvuna mamba.

"Tunaomba TAWA (Mamlaka ya Usimamisi wa wanyamapori) watoe kibali kwa wananchi cha kuwavuna mamba wakorofi,” amesema.

Kamonga pia ameiomba serikali kukamilisha mradi wa maji kijiji cha Kipingu kwa sababu awali kabla daraja la Ruhuhu halijajengwa wananchi walikuwa wanashambuliwa wakiwa wanavuka au kuchota maji.

Marehemu ameacha mume na watoto wawili.