Mwanamke jela maisha kwa kumbaka mtoto wa kiume

Muktasari:

Mahakama ya Rufani Tanzania imebariki kifungo cha maisha jela alichohukumiwa mwanamke mkazi wa Morogoro mjini, Shani Suleiman (35) kwa kosa la kumbaka mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12.


Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani Tanzania imebariki kifungo cha maisha jela alichohukumiwa mwanamke mkazi wa Morogoro mjini, Shani Suleiman (35) kwa kosa la kumbaka mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12.

Ushahidi unaonyesha mwanamke huyo alikamatwa baada ya mama mzazi wa mtoto huyo, akiwa na rafiki yake, kuandaa mtego katika nyumba ya mwanamke huyo ambapo walirekodi tukio hilo kwa kutumia simu janja.

Hii ni baada ya mtoto kumweleza mama yake kuwa mama Shani, maarudu kama Mama Shafii amekuwa akimwambia amwingilie mara kwa mara na wakati mwingine kinyume cha maumbile na mchezo huo aliufanya kwa miaka mitatu hadi mwaka 2019.

Hukumu ya Mahakama ya Rufani Tanzania ilitolewa Septemba 28, 2022 jijini Dar es Salaam na jopo la majaji watatu, Stella Mugasha, Mary Levira na Abrahaman Mwampashi, ilitupilia mbali rufaa ya mfungwa huyo.

Hii ilikuwa rufaa ya pili kutupwa baada ya ile ya kwanza ya kupinga hukumu ya kifungo cha maisha jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro 2019 kutupwa na Jaji Joaquine De-Mello wa Mahakama Kuu, Julai 28, 2021.

Katika rufaa yake ya pili ambayo ni ya mwisho kwa mfumo wa Tanzania, mshtakiwa aliegemea sababu moja kwamba upande wa mashtaka haukuwa umethibitisha shtaka hilo bila kuacha mashaka.

Pia aliegemea sababu nyingine kuwa umri wa miaka 12 wa mtoto huyo haukuthibitishwa, lakini hoja hizo zilipanguliwa vilivyo na wakili mwandamizi wa Serikali Christine Joas aliyesaidiana na wakili wa Serikali, Monica Ndakidemi.

Akijibu hoja kuwa shtaka halikuthibitishwa pasipo kuacha shaka, wakili Joas alisema shtaka lilithibitishwa na kwamba ushahidi wa shahidi wa pili ambaye ni mtoto huyo ulikuwa wa kuaminika na uliunganisha na nini alichofanyiwa.

Kuhusu suala la umri, wakili Joas aliirejesha mahakama kwenye ushahidi wa mama mzazi ambaye ni shahidi wa kwanza na mtoto mwenyewe, ambao unaonyesha kuwa wakati wa tukio hilo likitendeka alikuwa na umri wa miaka 12.

Wakitoa hukumu yao, majaji hao walisema baada ya kupitia kumbukumbu za kesi hiyo na hoja ya mshtakiwa kuwa shtaka halikuthibitishwa, wameona ni tofauti kabisa na kile anachokisema kwa kuwa kesi hiyo ilithibitishwa bila kuacha shaka.

Majaji hao walisema kwa kuutazama ushahidi, mshtakiwa alifanya kitendo hicho zaidi ya mara mbili na ushahidi wa mtoto uliunganika na wa mama na mashahidi wengine, hivyo mahakama imeridhika kuwa shtaka dhidi yake lilithibitishwa.

“Baada ya kubaini malalamiko ya mshtakiwa hayana msingi na kuyatupa, tunaridhika kesi dhidi ya mshtakiwa ilithibitishwa pasipo kuacha shaka na Jaji De-Melo alikuwa sahihi alipoitupa rufaa yake ya kwanza,” inasema hukumu hiyo.


Tukio lilivyokuwa

Ushahidi uliochambuliwa na majaji unaeleza kuwa siku moja mtoto huyo alimweleza mama yake kuwa “mama Shafii ananiambiaga nimfanye, nim (maneno hayaandikiki)”, kumaanisha mshtakiwa huwa anamshawishi wafanye mapenzi.

Baada ya mama mzazi kusikia hilo, alimshirikisha rafiki yake wa kike ili waweze kuandaa mtego wa kumkamata mshtakiwa ambapo Januari 13, 2019 akiwa na shoga yake huyo waliandaa mtego huo katika nyumba ya mshtakiwa.

Shoga yake huyo alienda katika nyumba ya mshtakiwa akiwa na simu janja na kujificha katika moja ya vyumba vya nyumba aliyokuwa akiishi mshtakiwa na kukaa eneo ambalo alikuwa akiona ndani ya sebule ya mshtakiwa.

Bila kujua, mshtakiwa alitokea na kumuuliza mtoto huyo kama angependa kufanya naye mapenzi muda ule, haraka haraka mshtakiwa alivua nguo na kukaa kwenye kochi na mtoto huyo akaja juu yake na wakaanza kufanya mapenzi.

Shahidi wa tatu ambaye ni rafiki na mama mzazi wa mtoto alirekodi kila kitu kwa kutumia simu janja, lakini baadaye mshtakiwa alimuona huyo mama na kubaini alikuwa anamrekodi, ndipo alivaa nguo harakaharaka na kwenda kupigana naye.

Shahidi huyo alipiga kelele na kuomba msaada na wananchi walijitokeza na kuwaamua na mtoto alipelekwa hospitali na kufanyiwa vipimo kisha mshtakiwa akakamatwa na kufunguliwa mashtaka hayo ya ubakaji na ulawiti.

Katika ushahidi wake alioutoa mahakamani, mtoto huyo alisema anakumbuka mwaka 2016 mshtakiwa alimwambia aingie ndani ya chumba chake na huko alichezea uume wake na baadaye aliuingiza na kufanya naye mapenzi.

Mchezo huo uliendelea siku zilizofuata na anakumbuka siku moja walikutana na mshtakiwa barabarani ambapo alimchukua na kumpeleka katika nyumba ambayo ilikuwa haijamalizika kujengwa ambapo alimvua nguo na kuchezea mwili wake.

Wakati huo anakutana naye alikuwa akisoma darasa la tano lakini mchezo huo waliuanza akiwa darasa la tatu.