Mwanamke mwenye miaka 56 adaiwa kumbaka mtoto wa miaka nane

Muktasari:

Mwanamke mwenye umri wa miaka 56 mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka nane.

Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Desderia Mbelwa mwanamke mwenye umri wa miaka 56, kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 8.

Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Allan Bukumbi amesema tukio hilo limetokea Mei 8, katika Kijiji Cha Lumuli, Wilaya ya Iringa Vijijini.

Amesema mwanamke huyo alimkamata kwa nguvu mtoto huyo kisha kumbaka na kumsababishia michubuko na maumivu makali sehemu zake za siri.

"Alimkamata kwa nguvu mtoto huyo anayesoma darasa la tatu alipokuwa anatoka shule na kumvutia kichakani," amesema Bukumbi na kuongeza;

"Baada ya kumvutia kichakani alimtishia asiseme na kufanya naye ngono kitendo kilichomsababishia mtoto huyo  maumivu makali na majeraha katika sehemu zake za  siri."

Bukumbi amesema Desderia amekiri kutenda kosa hilo bila kutaja sababu za yeye kufanya hivyo na atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.