Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwarobaini wa ‘kuwatuliza’ madaktari bingwa vituo vya kazi wapatikana

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu (wakwanza kulia) akikabidhi vifaa tiba alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Muktasari:

Serikali imesema imetafuta njia mbadala ya kuwafanya madaktari bingwa kubaki kwenye hospitali za Umma badala ya kukimbilia hospitali binafsi kwa kuwaruhusu kuwa na kliniki zao binafsi.

Shinyanga. Serikali imesema imetafuta njia mbadala ya kuwafanya madaktari bingwa kubaki kwenye hospitali za Umma badala ya kukimbilia hospitali binafsi kwa kuwaruhusu kuwa na kliniki zao binafsi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema utaratibu huo wa kutoa huduma binafsi kwa madaktari bingwa nje ya saa za kazi ambao  umekuwa ukifanyika hospitali ya Muhimbili, Jakaya Kikwete, Ocean Road na Moi, sasa utafanyika hadi hospitali za rufaa za mikoa ili kuwatuliza madaktari bingwa wabaki kwenye vituo vyao vya kazi.

Ummy aliyezungumza Julai 14, 2023 wakati wa ziara yake ya kukagua huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga amewatoa hofu wananchi akisema utaratibu huo hautoathiri utoaji wa huduma.

“Utaratibu huu ni mzuri na utavutia madaktari bingwa kufanya kazi hospitali za mikoani, hivyo niwatoe tu wasiwasi wananchi utaratibu huu hauta athiri utoaji wa wa huduma za afya badala yake utaboresha utoaji wa huduma za kibingwa katika maeneo yao,”amesema Waziri Ummy

Akizungumzia upungufu wa madaktari bingwa baada ya kupokea taarifa kuwa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga ina upungufu wa madaktari bingwa 15,  Waziri Ummy amesema tatizo hilo ni la nchi nzima.

Amesema Serikali ilitoa maombi ya ajira kwa madaktari bingwa 35 lakini waliomba 15, waliokidhi vigezo 11 na walioripoti kazini walikuwa sita pekee.

Awali akitoa taarifa kwa Waziri Ummy, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Luzila John amesema madaktari bingwa waliopo ni watano kati ya 20 wanaohitajika.

“Tuna upungufu wa madaktari bingwa 15 ila  watano wapo shule kusomea ubingwa na mwaka huu tunapeleka madaktari 5 kusoma. Kwa sasa kuna madaktari bingwa wawili wa magonjwa ya watoto,  wa magonjwa ya ndani ni mmoja, upasuaji mmoja na magonjwa ya kina mama mmoja,”amesema John

Amesema hospitali hiyo haina Mochwari akidai wanatumia mochwari iliyopo kwenye hospitali ya zamani ya mkoa huo ambapo mwaka wa fedha 2023/24 wanatarajia kujenga chumba hicho cha kuhifadhia maiti.

 Dk John ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo kwa  kutoa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo CT-SCAN na Digital X-RAY.

Katika ziara yake, Ummy amekagua utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wananchi pamoja na kukabidhi vifaa tiba kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi  kwa ajili ya kuokoa afya za watoto wachanga na njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

“Rais Samia ametoa Sh6.3 bilioni  kwa ajili ya kununua vifaa tiba nchi nzima, kwa ajili ya kuokoa afya ya watoto wachanga na njiti na leo hapa mkoani Shinyanga nakabidhi vifaa hivi vyenye thamani ya Sh170 milioni katika wodi ya watoto mahututi,”

“Vifaa hivi vitapelekwa pia katika hospitali ya Kahama na Kishapu. Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo mpya ya rufaa mkoani hapa na kuongeza majengo mengine, Rais Samia anataka kila mwanamke  mjamzito aondoke na kichanga chake kikiwa salama haijarishi kimezaliwa na uzito kiasi gani, ndiyo maana akatoa vifaa tiba,"amesema Waziri Ummy

Naye Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Paschal Ruggajo amesema utaratibu huo wa madaktari bingwa kufanya kazi zao binafsi nje ya saa za kazi katika Hospitali za umma utasaidia kuboresha pia huduma za kibingwa za dharura, sababu watakuwa muda wote katika vituo vyao vya kazi.