Mwigulu aeleza haya kuhusu tozo miamala ya simu

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema ukokotoaji wa hesabu kubaini kiwango watakachokubaliana na watoa huduma za simu ndio chanzo cha ucheleweshaji wa mchakato wa kupitia upya tozo za miamala ya simu kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema ukokotoaji wa hesabu kubaini kiwango watakachokubaliana na watoa huduma za simu ndio chanzo cha ucheleweshaji wa mchakato wa kupitia upya tozo za miamala ya simu kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwigulu ameeleza hayo leo Ijumaa Agosti 20, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Dar es Salaam kwamba katika tozo hizo, kiwango inachopata Serikali kutoka kwa mtumiaji wa simu ni kidogo ikilinganishwa na kile anachopata mtoa huduma akibainisha kuwa bado mazungumzo yanaendelea.

“Kilichokawiza mapendekezo ilikuwa namba, na hizi namba sio siri, zilivyokuwa zinasomeka wakati tumeziweka tulizikadiria kama zenyewe lakini pembeni kulikuwa na namba ambazo watoa huduma wanazipata kuanzia.”

“Na hapo kulikuwa na makundi mawili lakini jumla anayoipata mwananchi inakuwa na gharama zilizowekwa na mtoa huduma na zilizowekwa na Serikali,  ni  vizuri sana watanzania jambo hili walifikilie na walitafakari kama lao,” amesema.

Katika ufafanuzi wake Dk Mwigulu ameeleza, “mfano kama kuna eneo la watumiaji Serikali inachukua Sh 10 mtoa huduma anachukua Sh360, kwenye eneo ambalo Serikali inachukua Sh16, mtoa huduma anachukua Sh300, kwenye eneo ambalo Serikali inachukua Sh27, mtoa huduma anachukua Sh400, eneo ambalo Serikali inachukua Sh56, mtoa huduma anachukua Sh500, sehemu ambayo serikali inachukua Sh125, mtoa huduma anachukua 780 na kuendelea na kuendelea hizi mnazijua.”

“Sasa baada ya maelekezo kutaka ziangaliwe hizo namba, zikakamilika kuangaliwa upande mmoja, lakini hata ile kumi ikiondolewa na huku kuna 400, hivi uzito ni kweli hiyo 10, haya maumivu mzigo ni hii 10? Na kama hiyo 10 ndio unakwenda kujenga madarasa kwa hiyo kwenye hilo sisi tukasema hebu ngoja tuwaombe wananchi waendelee kuwa wavumilivu tujipe muda tuzungumze na wenzetu kwamba tulipojumlisha sisi na nyinyi huu mzigo umekuwa mkubwa kwa wananchi wetu hivi kweli hatuwezi kuangalia wote nani apunguze wapi.”

“Hivi pande zote mbili yaani Serikali na watoa huduma hili ni eneo ambalo linahitaji kuhusisha na watoa huduma hivi tuliwapa jukumu na wenzetu watafakari hivyo, ili tuje na njia mahususi,” amesisitiza

Amesema baada ya kikao hicho, kutakuwa na kikao kingine kitakachokamlisha shughuli hiyo na Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa atapanga kikao cha kupokea taarifa huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu.

Imeandikwa na Temaluge Kasuga,  Mwananchi
[email protected]