Mwigulu atoa ufafanuzi tozo za simu, majengo

Mwigulu atoa ufafanuzi tozo za simu, majengo

Muktasari:

  • Serikali imesema kuwa tozo za laini za simu ya Sh10 hadi Sh200 zitatozwa mara moja kwa mwezi kila mtu anapoongeza salio.

Dodoma/Dar. Serikali imesema kuwa tozo za laini za simu ya Sh10 hadi Sh200 zitatozwa mara moja kwa mwezi kila mtu anapoongeza salio.

Pia, imesema fedha za kodi ya majengo zitatozwa kwa mmiliki wa jengo kupitia luku.

Ufafanuzi huo umetolewa jana mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba alipokuwa akizungumza na wahariri kuhusu vyanzo vipya vya mapato alivyovisoma wiki iliyopita katika bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022.

Mwigulu alisema maeneo hayo hayajaeleweka vizuri ndiyo maana kumekuwa na mijadala mizito ndani na nje ya Bunge ambapo pia inahusisha tozo ya Sh100 kwa kila lita moja ya mafuta ya petroli na dizeli.

Alisema suala la kuongeza salio, atakayeweka Sh1,000 hadi Sh2,500 atakatwa Sh10 na atakayeweka Sh2,500 hadi Sh5,000 atakatwa Sh21. Yule atakayeweka Sh5,000 hadi Sh7,500 atakatwa Sh180. Yule atakayeweka Sh50,000 hadi Sh100,000 atakatwa Sh200.

Kuhusu kodi ya miamala atakayetoa Sh2000 atakatwa Sh10. Atakayetoa Sh10,000 hadi Sh15,000 atakatwa Sh300 huku atakayetoa Sh30,000 atakatwa Sh1,000. Yule wa Sh5 milioni na kuendelea atatozwa Sh10,000.

Kuhusu wapangaji alisema tozo kupitia luku itatozwa kwa wamiliki wa jengo hata kama nyumba ina wapangaji lukuki.

“Sisi tunaangalia jengo, kwa hiyo kama kuna mita 100 katika nyumba moja na anatakiwa kutozwa 100,000 basi fedha hiyo itachangiwa na wote. Haya mambo watu wa IT ndio wenye uwezo wa kuweka programu za kutoza na kukata fedha hizo,” alisema Mwigulu.

Wakati mjadala wa bajeti ukiendelea kushika kasi bungeni, Taasisi ya Wajibu jana imetoa mapendekezo katika maeneo yaliyoibua mjadala huku ikionyesha wasiwasi wa utekelezaji wa ukusanyaji wa kodi ya jengo kupitia luku.

Pamoja na kupongeza hatua hiyo, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Honest Ngowi alisema bado kuna mkanganyiko wa namna kodi hii itakavyokusanywa, hasa katika nyumba zenye luku zaidi ya moja na itakuwaje kwa zile wanazoishi wapangaji.

Akizungumza jana wakati wa kuchambua bajeti, Profesa Ngowi alisema: “Ukusanyaji huu una changamoto nyingi, nani atalipa mimi mwenye nyumba au mpangaji, kuna nyumba zina luku zaidi ya moja na sheria za kodi zinataka usawa, itakuwaje kwa nyumba moja ikatwe kodi kwenye luku tatu.

“Nyumba inayokaliwa na wazee inapaswa kuwa na msamaha, sasa kwa kigezo cha luku hata hawa watatakiwa kulipa, pia kuna aina za nyumba zipo zinazofanyiwa biashara, zisizofanyiwa hizi kodi zake haziwezi kuwa sawa,” alisema Profesa Ngowi.

Mbali na wasiwasi huo, Wajibu kupitia Mkurugenzi wake, Ludovick Utouh ilitoa mapendekezo kadhaa ili kuwezesha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa bajeti hiyo pendekezwa, ikiwamo Serikali kuongeza vyanzo vya mapato ili iweze kulihudumia deni la Taifa na kuimarisha uhusiano na nchi wahisani ili kupata misaada itakayosaidia utekelezaji wa bajeti.

Pia Serikali ianze majadiliano ya kuuza bidhaa na huduma za ziada zinazotokana na miradi ya kimkakati nje nchi ili kuhakikisha miradi hiyo inapokamilika inaanza kufanya kazi na kuliingizia fedha Taifa.

Akitolea mfano umeme utakaozalishwa kwenye bwawa la Nyerere na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), alisema ni muhimu huduma hizo zikaanza kutafutiwa soko ili itakapomalizika ianze kufanya kazi na kuiwezesha Serikali kupata fedha za kigeni za kuhudumia madeni yanayotokana na miradi hiyo.

Pia Serikali kufanya uwekezaji kwa kutambua na kutoza kodi biashara zinazofanyika kwa njia ya mtandao.

Salehe Mohamed na Elizabeth Edward, [email protected]