Mwili mwakilishi ACT-Wazalendo wazikwa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ameongoza mamia na wananchi na wafuasi wa chama hicho katika maziko ya Abubakar Khamis Bakari yaliyofanyika mjini Unguja leo Jumatano Novemba 11, 2020

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ameongoza mamia na wananchi na wafuasi wa chama hicho katika maziko ya Abubakar Khamis Bakari yaliyofanyika mjini Unguja leo Jumatano Novemba 11, 2020.

Bakari aliyekuwa mwakilishi mteule wa chama hicho jimbo la Pandani, Pemba amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Mbweni.

Swala ya jeneza imesaliwa katika msikiti wa Jamiatul Zinjibar uliopo Mazizini mjini Unguja.

Baadhi ya waliohudhuria maziko hayo ni Kadhi mkuu wa Zanzibar,  Sheikh Saleh Kaabi.

Akisoma wasifu wa Bakari, makamu mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Zanzibar,  Juma Duni Haji amesema marehemu alikua mtu mwenye msimamo na mpenda haki.

Amesema enzi za uhai wake walipigania umoja wa Wazanzibari na kwamba atakumbukwa kwa wema wake, akimtaja kama mmoja wa watu walioanzisha maridhiano Zanzibar.