Mzee Malecela ahani msiba wa Lowassa Monduli, atoa ng'ombe

Muktasari:

  • Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela amesema Wanamonduli wamempoteza kijana wao Edward Lowassa na kuwaomba kumwombea kheri.

Monduli. Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela na mkewe, Anne Kilango Malecela leo Jumamosi, Machi 23, 2024 wamefika Kijijini kwa Edward Lowassa, Ngarash, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha kuhani msiba wa Lowassa.

Wawili hao wamepokewa na wanafamilia wakiongozwa na mjane wa Lowassa, Mama Regina na watoto wake akiwemo Fredrick ambaye pia ni Mbunge wa Monduli.

Lowassa alifariki  Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu. Mwili wake ulizikwa Februari 17, 2024 kijijini Ngarash.

Baada ya Mzee Malecela na mkewe, Anne Kilango kuweka shada  la maua kwenye kaburi la Lowassa amesema, wananchi wa Monduli wamempoteza kijana mwema.

Malecela amesema hakuweza kufika wakati wa msiba kwani alikuwa nje ya nchi kwenye matibabu, hivyo baada ya kurejea nchini ameamua kufika Monduli kutoa pole.

Amesema Lowassa alikuwa kijana wake mwema na kwa Wakristo kifo ni hatua ya kwenda mbinguni hivyo familia na Watanzania wanapaswa kumuombea alazwe mahali pema peponi.

Malecela amesema katika kutoa pole kwa msiba huo, amemkabidhi ng’ombe mjane wa Lowassa, Mama Regina kutokana heshima ya kimila ya kigogo.

“Jamii ya Kigogo hutoa mnyama kama ishara ya pole ili nyama itakayotumika iweze kumfuta machozi kwa kumpoteza ndugu,” amesema.

Naye Mama Regina amemshukuru Mzee Malecela kwa kufika nyumbani kuwafariji akisema kitendo alichofanya ni cha thamani kubwa kwa familia yao, kwani ni heshima kusafiri umbali mrefu kufika kijijini na kutoa pole.

“Imani inatutuma kwamba Mungu alitupa thamani ya baba mwema Edward na umefika wakati baba wa mbinguni amemchukua na kwenda kumpumzisha mahala pema… tunamuomba Mungu atuimarishe ili tusimame imara kama familia,” amesema Regina.

Amesema Edward ameondoka lakini amewaachia marafiki wengi, akiwepo Mzee Malecela na wengine ambao wamekuwa faraja kwa familia.

Naye mtoto wa kwanza wa Lowassa, Fredrick amemshukuru Mzee Malecela kufika Ngarash kutoa pole kwani ni kiongozi ambaye amewahi kufanya kazi kwa karibu zaidi na baba yake.

Amesema Mzee Malecela alipokuwa Waziri Mkuu (Novemba 1990-Desemba 1994), ndiye alikuwa kiongozi wa kwanza kumteua Edward Lowassa kuwa msaidizi wake serikalini, na wakati wote amekuwa na uhusiano mzuri na familia ya Lowassa.

Amemshukuru pia Anne Kilango Malecela ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa kuendelea kumlea bungeni, lakini pia kuendelea kumtunza Waziri Mkuu mstaafu John Malecela.