Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Naibu waziri akutana na madudu kwenye kiwanda cha Wachina

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde

Muktasari:

Raia wa kigeni wanafanya kazi ambazo Watanzania wanao uwezo wa kuzifanya

Dodoma. Serikali imeamua kukifunga kiwanda cha mbao nyepesi kinachomilikiwa na raia wa China kutokana na mazingira yake kutokuwa salama kwa wafanyakazi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde alifikia uamuzi huo juzi, baada ya kukitembelea kiwanda hicho cha S & Y Company Ltd na kukitoza faini ya Sh4 milioni.

Kadhalika, katika tukio hilo raia 10 wenye asili ya nchi hiyo walitakiwa kujisalimisha Uhamiaji.

Mavunde alichukua uamuzi huo juzi katika kiwanda hicho kilichopo Zuzu nje ya Mji wa Dodoma, baada ya kukitembelea na kushuhudia idadi kubwa ya raia wa kigeni ambao wanafanya kazi bila ya kuwa na vibali.

Kiwanda hicho ambacho kinatengeneza mbao nyepesi, upande mwingine kinatumika kama machinjio na kiko katika mazingira machafu.

Alipofika kiwandani hapo, Mavunde alikutana na walinzi ambao walimzuia kuingia ndani hata baada ya kujitambulisha hadi msaidizi wake alipotumia nguvu kufungua geti.

Hata hivyo, raia hao walipobaini ameingia, waliwasha magari na kuanza kukimbia kabla ya kuzuiwa getini na wasaidizi wa waziri.

Kiwanda hicho kilibainika kuwa na wafanyakazi zaidi ya 80 wa Kitanzania na raia 10 wa China, lakini mazingira yake ni hatarishi kwa afya zao na hakuna mfanyakazi aliyeonekana kuwa na vifaa vya usalama.

Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho aliyejitambulisha kwa jina la Su, alikiri kuwapo kwa upungufu kwa mujibu wa sheria za kazi, lakini akasema atarekebisha.

Meneja Msaidizi wa kiwanda, Titus Gembe alisema kilianza uzalishaji Novemba, 2015 na kukikiri kwa waziri kuwa hakuna mfanyakazi aliyepewa vifaa vya kazi na wote hawana mikataba pamoja mazingira kuwa hatarishi.

Alipoulizwa ni kwa nini watu wanafanya kazi kwenye mashine kubwa lakini hawana hata kandambili za kuvaa? Meneja huyo aliomba msamaha kwa naibu waziri na kumsihi asikifunge kiwanda hicho.

Jirani na kiwanda hicho kuna kiwanda cha Sunshine Industrial, ambako alikutana na raia wa China waliojisajili kama mafundi lakini wanafanya kazi ya kufagia.

Kiwanda hicho ambacho kinazalisha mafuta ya kula ya alizeti, kilibainika kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi ambao hawana mikataba.

Kaimu Ofisa Kazi Mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma, Jacob Mwinula alisema viwanda hivyo ni sehemu ya vingine vingi ambavyo vinafanyakazi kinyume cha sheria.

Alisema kitendo hicho kinawafanya raia wa Tanzania kukosa kazi, huku idadi ya viwanda ikielezwa kuwa kubwa.