Nakisi yatishia uhai wa NHIF

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imesema imebaini Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatengeneza nakisi katika mapato na matumizi, jambo ambalo linatishia uhai wa mfuko.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imesema, imebaini Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatengeneza nakisi katika mapato na matumizi, jambo ambalo linatishia uhai wa mfuko.

 Mwenyekiti wa PIC, Jerry Silaa ameyasema hayo leo Alhamis Agosti 25, 2022 baada ya kupokea taarifa ya uwekezaji na hesabu za mfuko huo.

Amesema baada ya kufanyia uchambuzi taarifa hizo, kamati imeelekeza NHIF kufanya mchakato kwa kuongeza wanachama kwa sababu malipo ya huduma za wanachama yamekuwa yakiongezeka ukilinganisha na mapato yanavyoongezeka.

“Kwa hiyo gharama zinaongezeka kuliko mapato na hii inahatarisha uhai wa mfuko kwa hivyo kamati imeelekeza ifanye juhudi za makusudi za kuongeza wanachama,” amesema Silaa.

Pia, amesema wameuagiza mfuko huo kuwa na jitihada za makusudi za kuhakikisha kuna utaratibu mzuri wa kuthibiti matumizi.

Amesema kamati imeelekeza mfuko huo kuboresha mifumo ya Tehama kwasababu wameona kuna mapungufu ya mifumo ya Tehama.

Amesema kama NHIF itaimarisha mifumo yake ya Tehama kwenye majukumu yake yote manne wanaweza kupunguza udanganyifu na mapato yao yakaongezeka.

Ameyataja maeneo hayo ni uandikishaji wanachama, wanapopata huduma kwenye vituo vya kutolea huduma kuhakikisha mwanachama anapata huduma madhubuti inayoendana na uanachama wake pamoja na maradhi anayoumwa na udahili wa madai ya watoa huduma.

“Yote haya yakiwa katika mfumo, matumizi ambayo yanaonekana yana aina fulani ya udanganyifu yatapungua na mapato yataongezeka ili uweze kuhudumia wanachama wake wote,” amesema.

Amesema NHIF ikiendelea kuwa na nakisi katika mapato na matumizi kila mwaka kunaweza kusababisha mfuko huo kula mtaji uhai wa shirika ndio maana amesema uhai wa shirika unaanza kutishika.