Nanenane kushirikisha wakulima 200,000 Nyanda za Juu Kusini
Muonekano wa nje wa ujenzi wa moja ya lango kuu la kuingia viwanja vya John Mwakangale vitakavyo tumika katika maonyesho ya sikukuu ya wakulima nanenane Mkoa wa Mbeya na kuhusisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Muktasari:
- Imeelezwa idadi ya wakulima imeongezeka kutoka 150,000 msimu uliopita hadi 200,000 sawa na ongezeko la wakulima 50,000.
Mbeya. Zaidi ya wakulima 200,000 kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wanatarajiwa kushiriki Maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) yatakayofanyika Agosti 8, 2026, katika Viwanja vya John Mwakangale, mkoani Mbeya.
Idadi hiyo ni ongezeko la wakulima 50,000 ikilinganishwa na washiriki 150,000 walioshiriki maonyesho hayo mwaka jana.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Julai 2, 2026, Mratibu wa Maonyesho ya Nanenane Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Meneja wa Viwanja vya John Mwakangale, Saimon Parmet, amesema maandalizi ya miundombinu yamefikia zaidi ya asilimia 90.
"Mwaka jana maandalizi hayakuwa mazuri kutokana na ujenzi wa miundombinu kuendelea. Mwaka huu kazi nyingi zimekamilika na mkandarasi akiwa katika hatua za mwisho za ukarabati wa barabara za ndani na ujenzi wa uzio ukikaribia kukamilika," amesema.
Amesema zaidi ya taasisi na kampuni 300 tayari yamethibitisha kushiriki, huku halmashauri 47 kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini zikitarajiwa kushiriki maonyesho hayo.
"Tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa uwekezaji uliofanyika katika kuboresha Viwanja vya John Mwakangale. Maboresho haya yameongeza hamasa ya ushiriki wa wakulima na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo," amesema.
Akizungumzia maandalizi hayo, mkulima Kamwela Joel amesema, "Tunaomba mwaka huu Serikali na taasisi za utafiti zitoe elimu zaidi kuhusu mbegu zinazostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamekuwa changamoto kubwa kwa uzalishaji wa mazao, hususan viazi mviringo.”
Kwa upande wake, mfanyabiashara katika Kituo cha Mabasi cha Nanenane, Zainad Hashim amesema maonyesho hayo yameendelea kuwa fursa muhimu ya kiuchumi kwa wafanyabiashara kutokana na kuongezeka kwa shughuli za biashara na idadi ya watu wanaotembelea.