Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nauli za usafiri wa majini Dar–Zanzibar zapaa, Tasac yapiga jaramba

Muktasari:

  • Sasa abiria wa daraja la kawaida atakuwa akilipa Sh40,000 badala ya Sh35,000, huku abiria wa VIP akilazimika kulipa Sh80,000 kutoka Sh70,000 waliyokuwa wakilipa awali.

Unguja. Maumivu ya ongezeko la bei ya nauli sasa yanahamia katika usafiri wa majini kwa watu wanaofanya safari za Zanzibar na Dar es Salaam kuanzia kesho Mei 8, 2026.

Hiyo ni baada ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kutangaza nauli mpya za boti, huku Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) likisema nauli za safari za meli katika maziwa ya Tanzania Bara zitatangazwa hivi karibuni.

Zanzibar na Tanzania Bara zinaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazoshuhudia athari hasi za ongezeko la bei za mafuta, kutokana na vita inayoendelea Mashariki ya Kati, ambayo imepelekea mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji wa mafuta.

Kutokana na hali hiyo, sasa abiria wa daraja la kawaida watalipa Sh40,000 kutoka Sh35,000 waliyokuwa wakilipa awali, huku wa daraja la VIP wataanza kulipa Sh80,000 kutoka Sh70,000 waliyokuwa wakilipa awali.

Nusu tiketi itauzwa kwa Sh20,000, na bei ya Flying Horse imetoka Sh20,000 hadi Sh22,000. Hata hivyo, watumiaji wa boti kutoka Unguja kwenda Pemba wataendelea kulipa Sh40,000 na Pemba kwenda Tanga Sh30,000.

Taarifa iliyotolewa na ZMA na kuthibitishwa na ofisa habari wa mamlaka hiyo, Suleiman Salim, imeeleza kuwa ongezeko hilo linatokana na bei ya mafuta kuwa juu.

“Ni sahihi, nauli zimepanda na zitaanza kutumika rasmi kesho (Mei 8, 2026). Mamlaka inalitambua hilo,” amesema.

Bei hizo mpya ni kwa ajili ya boti za abiria ziendazo kwa kasi pamoja na boti ya Flying Horse tu, na hazitahusisha meli za mizigo na abiria ziendazo taratibu.

“Mamlaka inawataka wamiliki wa vyombo kuzingatia bei hizi, na pia inawaomba wananchi kununua tiketi katika ofisi za kampuni au mawakala wanaotambulika, na kuacha kununua tiketi za ulanguzi,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Hili linafanyika ikiwa ni muda mchache tangu Zanzibar kutangaza ongezeko la bei ya bidhaa za mafuta, ambapo sasa lita moja ya petroli itauzwa kwa Sh3,820 kutoka Sh3,500 iliyokuwapo Aprili mwaka huu, sawa na ongezeko la Sh320, huku dizeli na mafuta ya taa zikiuzwa kwa Sh3,850 ikilinganishwa na Sh3,500 iliyokuwapo mwezi uliopita.

Wakati Zanzibar hali ikiwa hivyo, kwa upande wa Dar es Salaam sasa lita moja ya petroli Mei mwaka huu inanunuliwa kwa Sh4,115 kutoka Sh3,820; dizeli Sh4,248 kutoka Sh3,806, huku mafuta ya taa sasa yatanunuliwa kwa Sh4,677 kutoka Sh3,684 iliyokuwa ikitumika Aprili mwaka huu.

Mmoja wa wakatisha tiketi kutoka Kampuni ya Zan Fast Ferries amesema hadi sasa kampuni hiyo haijatoa taarifa ya ongezeko la nauli, ingawa wanatarajia kutokea hilo wakati wowote kwa Dar es Salaam kuja Zanzibar na si kutoka Unguja kuelekea Pemba.

“Kwa sasa kampuni yetu bado haijatoa taarifa rasmi ya ongezeko la nauli. Tunatumia hiyo ya Sh35,000 na Sh60,000 kwa VIP,” amesema.

Akizungumza baada ya ongezeko hilo, mwananchi Hinaya Mansour Mahmoud amesema anashangazwa kuona kila mwaka bei za nauli zinapanda bila kuangalia hali za wananchi.

Amesema mwaka juzi nauli ilikuwa Sh30,000 kutoka Zanzibar hadi Dar, na sasa imeshaongezwa tena kufikia Sh40,000, hawajui lengo hasa la vyombo hivyo vya usafiri kupandisha bei.

Amefafanua kuwa wachache watakuwa na uwezo wa kumudu gharama hizo, na wengi watasitisha safari zao kwa kushindwa kumudu hilo.

“Huku tunakoelekea ni kubaya. Wananchi tuna hali duni, na kila siku unaambiwa nauli zimepanda. Hatuelewi lengo la kupandishwa kwa nauli hizo kila baada ya mwaka,” amesema.

Mwananchi mwingine, Kombo Himidi, amesema kupanda kwa nauli hizo kumekatisha matumaini ya wananchi wengi, hususan wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara za kusafiri.

Wakati nauli zikipanda upande wa Zanzibar, kwa upande wa vyombo vya majini vilivyopo katika maziwa mbalimbali ya Tanzania Bara, nauli mpya ziko mbioni kutangazwa.

“Tunatarajia kutangaza nauli mpya kwa vyombo vya majini Tanzania Bara. Mchakato umeshafanyika na umekamilika, na sasa tunachokisubiri ni ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wachapishe,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Malick Salum.