Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari za boti Dar - Zanzibar zarejea

Muktasari:

  • Kampuni ya Azam Marine imeanza kurejesha usafiri wa boti kutoka Dar kuelekea Zanzibar huku ikiendelea kufuatia hali ya bahari kabla ya kuruhusu boti kutoka Zanzibar kuanza safari

Dar es Salaam. Usafiri wa boti za Azam Marine kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar umerejea mapema leo asubuhi Alhamisi Oktoba 25, 2018.

Boti ya Kilimanjaro yenye uwezo wa kubeba watu 520 imeondoka saa moja asubuhi ikiwa na abiria 300 pekee.

Usafiri huo umerejea baada ya taarifa za hali ya hewa hadi jana Jumatano kuonyesha hali ya bahari inaruhusu vyombo vya baharini kusafiri.

Ofisa anayehusika na usalama wa boti za Azam Marine, Kepteni Feruzi Kassim amesema  kwa mujibu wa taarifa za hali ya hewa urefu wa mawimbi umepungua kutoka mita 4 ya juzi hadi kufikia mita 3.3 jana.

Amesema hali inaonekana shwari zaidi kutokea Dar es Salaam kuliko ilivyo upande wa Zanzibar.

Amesema hilo linatokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyotokea usiku wa jana kuanzia saa nane hadi saa 10 alfajiri kufuatia kuvuma kwa upepo na mvua iliyonyesha.

“Kutoka Dar hakuna shida kwa sababu boti inasukumwa kwenda mbele na tumejiridhisha kwamba hakuna shida boti ya kwanza imeondoka na tumechukua abiria wachache kwa sababu ya usalama ili chombo kisiwe kizito,” amesema Kassim.

Kuhusu upande wa Zanzibar, Kassim amesema bado hajapata taarifa ingawa kutokea huko kuna eneo linaweza kuleta usumbufu na kukipa wakati mgumu chombo kutembea kwenye mawimbi makubwa.

Amesema kikosi kilichoondoka na boti ya kwanza kutoka Dar watatoa taarifa kuhusu hali ya eneo hilo ili kuona kama wanaweza kuruhusu boti kutoka Zanzibar kuanza safari.

“Acha nifuatilie nijue nini kinaendelea na kama chombo kitatoka halafu wakakuta bahari imechafuka itabidi warudi kwa sababu hali ya hewa inaweza kubadilika wakati wowote,” amesema Kassim.