Ndege ya ATCL yakodiwa kupeleka mzigo Afrika ya Kati

Rubani kiongozi wa Ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege Tanzania, (ATCL) Mbarouk Mbarouk
Muktasari:
- Muhtasari Ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), inatarajiwa kufanya safari isiyokuwa na ratiba maalumu kwenda nchi ya Afrika ya Kati kupeleka mzigo.
Dar es Salaam. Ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), baadaye leo inatarajiwa kufanya safari isiyokuwa ya ratiba maalumu kwenda nchi ya Afrika ya Kati kupeleka mzigo.
Ndege hiyo aina ya Boeing 767-300F hadi sasa imeshafanya safari mbili kwenda Dubai ikiwemo ile ya Julai 10, mwaka huu.
Ikitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julias Nyerere (JNIA) ndege hiyo inaenda Afrika ya Kati kupeleka mzigo baada ya kukodiwa.
Akizungumza Dar es Salaam, katika shughuli ya kupakia mizigo kwenye ndege hiyo, Rubani wa Ndege hiyo, Mbarouk Mbarouk amesema wanafanya safari hiyo baada ya kukodiwa.
"Safari yetu itadumu kwa masaa matatu na dakika 1, (3:10) na sasa tunafanya Maandalizi ya mwisho katika kupakia mizigo,tumejiandaa vizuri na tumejipanga kuona tunafika mbali zaidi," amesema Mbarouk
Katika maeelezo yake rubani huyo amesema anarusha ndege hiyo kwa mara ya pili huku akisema safari yake ya kwanza alienda Zanzibar na kurudi.
"Tangu ndege hii imenunuliwa muitikio umekuwa mkubwa kwani oda za kuikodi kwaajili ya kusafirisha mizigo ni nyingi, na pia wafanyabiashara kutoka mataifa ya China, Mumbai India na Dubai muamko wao ni mkubwa wa kuhitaji huduma," amesema.
Julai 10, Mwaka huu, wakati ndege hiyo inasafiri kwenda Dubai, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni hiyo, Patrick Ndekena alisema ratiba ya safari za Dubai itakuwa mara mbili kwa wiki (Ijumaa na Jumatatu).
Alisema azma ya ATCL ni kuhakikisha bidhaa za wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi zinafika kwa wakati na zikiwa na ubora wake kwenye nchi mbalimbali kwa kadri ya inavyotakiwa.
“Leo tunafuraha kubwa kwa kuanza rasmi safari zetu za ratiba kwa ndege yetu hii mpya ya mizigo Boeing 767-300F yenye uwezo wa kusafiri masafa marefu na uzito mkubwa yaani tani 54 kwa mara moja,” alisema Ndekena
Alifanua kuhusu uwezo wa ndege hiyo alisema nitoleo la kisasa, ina uwezo wa kwenda mwendo wa kilometa 850 kwa saa na kukaa angani kwa zaidi ya masaa 10 bila kutua.