Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndejembi aonya matumizi mabaya ya Sh800 milioni za hospitali

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Deogratius Ndejembi akisalimiana na wageni  wakati kamati ya Bunge ya Tamisemi, ilipotembelea ujenzi wa jengo la utawala, mionzi, kufulia na jengo la kutolea dawa yanayojengwa katika hospitali ya Wilaya ya Moshi. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Deogratius Ndejembi ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kuhakikisha fedha zilizotolewa na Serikali zaidi ya Sh800 milioni kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne yanayojengwa katika hospitali ya wilaya hiyo zinatumika ipasavyo.

Moshi. Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Deogratius Ndejembi ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kuhakikisha fedha zilizotolewa na Serikali zaidi ya Sh800 milioni kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne yanayojengwa katika hospitali ya wilaya hiyo,  zinatumika ipasavyo.

Majengo hayo ambayo ni jengo la utawala, mionzi, kufulia na jengo la kutolea dawa,  ujenzi wake  upo katika hatua za awali ambapo ujenzi wake  ulianza Februari mwaka huu na mpaka sasa zimeshatumika zaidi ya Sh40 milioni.

Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Alhamisi Machi 14, 2024 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikitembelea mradi huo.

"Nimepokea maoni na maelekezo yaliyotolewa na kamati hapa, niahidi tunakwenda kushughulikia yale yote ambayo yamesemwa hapa. Niwatake watalaam wetu, Mkurugenzi wa Halmashauri na jopo lake lote, kuhakikisha kila fedha iliyokusudiwa kujenga majengo haya ifanye kazi hiyo.

"Na wale watakaokuwa hapa wasimamie kwa weledi wa hali ya juu ujenzi huu, ili kamati ikirudi kuja kuangalia isije ikakuta hayajaisha au kuambiwa kuna fedha haijakamilika," amesema Ndejembi.

Ndejembi pia amemwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani hapa, Nicholus Francis kuhakikisha kipande cha barabara kinachoingia hospitalini hapo, kinafanyiwa tathmini ya haraka ili barabara hiyo iweze kutengenezwa mapema na wananchi waweze kufika hospitalini hapo kwa wepesi.

Amesema Serikali ya awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi katika hospitali hiyo, hivyo wananchi ni lazima waboreshewe miundombinu ya barabara ili waweze kupata huduma bora na nzuri inayotakiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Denis Londo ambaye ni Mbunge wa Mikumi, amesema changamoto zote ambazo wameziona katika miradi ya afya,  wataenda kuzifanyia tathmini na kuzitolea ripoti ya jumla.

"Changamoto ambazo tumeziona kwenye miradi hii ya afya tutakwenda kufanya majumuisho na tutatoa ripoti ya jumla ya kamati, lakini kuna mambo ambayo idara ya afya inatakiwa iangalie hasa kwa utekelezaji wa miradi hii mikubwa," amesema Londo.

Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe ambaye pia amemwakilisha Mbunge wa Moshi vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, ameiomba Serikali kutafuta fedha ya dharura ili kuhakikisha barabara hiyo muhimu ya kuelekea hospitalini hapo inatengenezwa.

"Nikuombe sana waziri wetu, hii barabara inayotoka hapa hospitalini, tusaidie tupate hii barabara kwa sababu ina kuja eneo la huduma na ikifunguliwa kutakuwa na huduma mbalimbali za kijamii hapa," amesema Mafuwe.

Akizungumza wa niaba ya wananchi wa Kata ya Mabogini, Diwani wa kata hiyo, Bibiana Massawe, amesema kumekuwepo na changamoto kubwa ya barabara kutopitika hasa katika kipindi cha mvua  na kwamba imekuwa ni kilio cha muda mrefu.