Ndingo aomba wananchi wamkopeshe imani

Mgombea ubunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kujinadi uliofanyika Kijiji cha Mwanavala katika Kata ya Imalilo- Songwe wilayani Mbarali mkoani Mbeya
Muktasari:
- Septemba 19, mwaka huu wananchi wa Mbarali watapiga kura ya kumchagua mbunge atakayeziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega aliyefariki dunia Julai Mosi huku Bahati Ndingo akiwaomba wamkopeshe imani.
Mbarali. Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbarali kwa tiketi ya CCM, Bahati Ndingo amewataka wakazi wa Mbarali kuitumia vema siku ya Septemba 19, 2023 ambayo utafanyika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kwa kumchagua awe mbunge wao ili amalizie ungwe iliyobaki kwa kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi hao ni Tangazo la Gazeti la Serikali namba 28 la mwaka 2008 linalowazuia kufanya shughuli za kudumu za maendeleo katika baadhi ya maeneo ili kulinda vyanzo vya maji, mto Ruaha na bonde la Ihefu.
Ndingo ametoa kauli hiyo leo Jumapili Septemba 17, 2023 wakati akiomba kura kwa wananchi wa vijiji vya Magwalisi, Mwanavala na Warumba ambapo amewaomba wamchague yeye ili achochee maendeleo.
Keshokutwa, wananchi wa Mbarali watapiga kura ya kumchagua mbunge atakayeziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega aliyefariki dunia Julai Mosi baada ya kugongwa na trekta dogo (Power Tiller) akiwa shambani kwake.
Ndingo aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu na kujiuzulu baada ya Kamati Kuu ya CCM kupitisha jina lake la kuwania nafasi ya ubunge Mbarali amewataka wananchi hao kutofanya makosa ya kumchagua mtu mwingine zaidi yake.
"Ndugu zangu mkiwemo wanakijiji cha Mwanavaka keshokutwa (Jumanne) nendeni mkafanya uamuzi sahihi wa kunichagua niwe mwakilishi wenu. Nataka tuendeleze pale alipoishia mtangulizi wetu (Mtega), sitowaungusha.
Nikopesheni imani nije kulipa kazi, tumebakiwa na siku moja kufanya uamuzi wa kupata sauti ya wananchi wa Mbarali, sasa twendeni tukamchague Bahati awe sauti yenu. Niko tayari kuwatumikia kwa ushirikiano na viongozi wa ngazi zote," amesema Ndingo.
Katika mkutano wa uliofanyika Mwanavala, Ndingo alitoa fursa kwa wananchi kuuliza maswali au maoni, ambapo mkazi wa kijiji hicho, Isaya Oleseseni alimhoji atawasaidiaje kuhusu changamoto yaTangazo la Serikali la mwaka 2008.
Akijibu hoja hiyo, Ndingo alimwakikishia Oleseseni kwa kumwambia Serikali ni sikivu na jambo hilo linafaihamika huku akimweleza kuwa hivi karibuni kwa msisitizo alifikisha kilio hicho kwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mizengo Pinda (Waziri mkuu mstaafu) na Dk Spika wa Bunge Tulia Ackson.
Katika mikutano ya kampeni hizo, Ndingo aliambatana na baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM na mbunge wa Iringa, Mjini Jesca Msavatavangu aliyewataka wananchi wa Mbarali kutokuwa na wasiwasi mgombea huyo kwa anajua shida zao.