Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndoa, imani za kishirikina zatwajwa chanzo cha ukatili

Klabu ya Tuwalinde katika shule ya Msingi Mramba, iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanharo.

Muktasari:

  • Klabu za wanafunzi za Tuwalinde, ambazo zimeanzishwa chini ya mradi wa kulinda watoto unaofadhiliwa na shirika la PROBONO la nchini Ujerumani, zimesaidia kutoa elimu kwa watoto na kuibua changamoto na visababishi vya vitendo vya kikatili katika jamii.

Mwanga. Mila na desturi, imani za kishirikina pamoja na kuvunjika kwa ndoa, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea vitendo vya kikatili dhidi ya watoto ikiwemo, ubakaji, ulawiti na hata mimba na ndoa za utotoni.

Hayo yamebainishwa na mratibu wa miradi katika shirika lisilo la kiserikali linalohusika na kutoa msaada wa kisheria kwa jamii na kutetea haki za binadamu (Ajiso) Tatu Mrutu wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Mwaka mmoja, tangu kuanzishwa kwa klabu ya Tuwalinde katika shule ya Msingi Mramba iliyopo Wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Mrutu amesema Klabu za wanafunzi za Tuwalinde, ambazo zimeanzishwa chini ya mradi wa kulinda watoto unaofadhiliwa na shirika la PROBONO la nchini Ujerumani,  zimesaidia kutoa elimu kwa watoto na kuibua changamoto na visababishi vya vitendo vya kikatili katika jamii.

Amesema kupitia mradi huo, wanafunzi wameweza kuibua baadhi ya vichocheo vya ukatili kwa watoto ikiwa ni pamoja na mila na desturi ambapo baadhi ya familia wameziendekeza na kuumiza watoto.

"Mila na desturi bado zimejikita katika jamii yetu na hii ni changamoto ambayo bado tunaipigia kelele, mfano wachaga hupenda kutumia jani la Sale kusuluhisha matatizo hata ya ukatili kama ubakaji na ulawiti wanayamaliza kifamilia na kuwaumiza watoto"

"Lakini wapare wao wana kitu wanaita Mbuta, yaani mzazi anakuwa ameshapewa hela na kijana kwamba huyu atakuwa mke wangu hivyo anashindwa kumzuia kijana kuja nyumbani kumfuata binti na inakuwa ngumu kuzuia ukatili na hata ndoa za utotoni, tunaona ni namna gani watoto wataendelea kuumia na kuteseka, kama hatutapiga kelele, na kupinga mila hizi ambazo hazifai".anesema Mrutu.

Ameongeza kuwa "Lakini pia ipo changamoto ya ndoa kuvunjika na watoto kulelewa na wababa wa kufikia(Baba wa Kambo) kwani tumepokea kesi nyingi za hawa wababa kuwafanyia ukatili mabinti wa wake zao hadi kuwapa ujauzito na kutokana na vitisho ambavyo hutolewa kwa watoto, huogopa kusema na kubaki na maunivu".

Aidha amesema kupitia mradi wa kuwalinda watoto, wameendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia klabu za wanafunzi zilizoanzishwa na katika kipindi cha mwaka mmoja watoto wameweza kuwa na uthubutu na kueleza madhila wanayopitia katika familia na hata kwenye jamii.

"Mradi huu wa  kulinda watoto, ulianza miaka mitatu iliyopita katika maeneo mbalimbali, lakini kwa hapa Mwanga tuliuanzisha Mwaka jana katika Shule ya msingi  Mramba na Reli juu , ambapo tulianzisha klabu za tuwalinde zenye wanafunzi 20 kwa kila shule, na tulilenga kuwawezesha wanafunzi kutoa elimu na kuibua matatizo yanayowapata wenzao katika jamii na kuyatolea taarifa".

"Klabu ya tuwalinde zimeweza kuwajengea wanafunzi ujasiri na uthubutu wa kueleza yale wanayofanyiwa nyumbani na maeneo mengine bila woga kwani wamekuwa wakitishiwa na kuogopa kusema".

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Klabu ya Tuwalinde katika Shule ya msingi Mramba, mwenyekiti wa klabu hiyo Sayuni Hilary ambaye ni mwanafunzi shuleni hapo,  amesema wamekuwa na utaratibu wa kuwa na mada ya kujadili kwa njia ya mdahalo kila wiki ili kufikisha ujumbe kuhusu changamoto zinazowakabili watoto na kuzitafutia ufumbuzi.

"Wiki ya Kwanza tulikuwa na mada ya kutokomeza utoro, ambapo tuliandaa mdahalo, ngonjera, mashairi, nyimbo na maigizo, ikafuata kutokomeza ukatili kwa watoto, Elimu ya kujitegemea ambapo tumeanzisha bustani za mboga, lakini pia tuliitisha mkutano wa wazazi na kuhamasisha watulipie fedha za chakula cha mchana".

"Yaani Kila wiki tunakuwa na mdahalo unaozungumzia ukatili, na tangu kuanzishwa kwa klabu hii, tumeweza kubaini watoto Sita waliofanyiwa vitendo vya ukatili majumbani ambapo wasichana ni wanne na wavulana wawili,   tuliwaripoti kwa walimu ambapo wamesaidiwa".

Amesema pamoja na mafanikio waliyopata pia wamebaini vitendo vingi vya kikatili wanavyofanyiwa watoto, vinafanywa na ndugu wa karibu wanaowaamini, ambapo pia huwatisha kutoa taarifa na matatizo kumalizwa kifamilia.

"Changamoto nyingine iliyopo, ni kuwepo kwa wimbi kubwa la wanafunzi ambao hawajalipiwa chakula cha mchana shuleni, kwani kati ya wanafunzi 655 wa kutwa waliolipiwa chakula ni 93 pekee, lakini pia lipo tatizo la wazazi kusuluhisha kesi za ubakaji na ulawiti nyumbani na ajira za utotoni, tunaamini kupitia Klabu hii, tunaweza kujenga uelewa jwa wenzetu na kupunguza changamoto".