Ndugai: Nitastaafu ubunge, siasa nimo

Muktasari:

  • Asema ataendelea kukitumikia chama popote
  • Asema angetamani kuona wengine wanafanya nini.

Dodoma. Spika wa zamani wa Bunge, Job Ndugai amesema mwaka 2025 atastaafu ubunge lakini si siasa.

Ndugai ambaye pia mbunge wa Kongwa ametoa kauli hiyo baada ya juzi kutangaza kutogombea ubunge uchaguzi mkuu 2025 akiwa kwenye ibada katika Kanisa la Anglikana Pareshi ya Matakatifu Michael Kongwa wakati waumini walipokabidhi gari walilolinunua kwa ajili ya shughuli za kanisa.

Akizungumza na Mwanachi jana kwa simu alisema itakapofika mwaka 2025 atakuwa ameongoza jimbo hilo kwa miaka 25, hivyo angetamani kuona wengine wanafanya nini.

“Sijasema naacha siasa, ila naacha kugombea lakini chama changu kikinituma kazi popote nitakwenda kuifanya hadi hapo Mungu atakapoamua vinginevyo,” alisema Ndugai.

Kuhusu kauli yake kuitolea kanisani, alisema haikuwa na tatizo, kwani alitumia nafasi hiyo baada ya kusikia Askofu wao, Dk Jacob Chimeledya kutangaza kustaafu ifikapo Agosti mwaka huu.

“Mimi ni muumini wa hapo, nilimsikia Askofu wangu Chimeledya akisema anataka kupumzika itakapofika mwezi wa nane, ndipo wakati wa kusalimia nami nikasema wakati wangu ukifika siendelei, nataka kupumzika,” alisema Ndugai. Katika Kanisa la Anglikana, Ndugai amepewa cheo cha Rey Canon ambacho hupewa watu wenye busara hata za kumshauri askofu kwa jambo lolote na mara nyingi huwa ni wachache kanisani.

Kwa mara ya kwanza, Ndugai alitoa kauli kama hiyo mwaka 2020 baada ya kutangazwa kupita bila kupingwa akisema hicho kitakuwa kipindi chake cha mwisho. Katika uchaguzi wa 2015 ilisambaa video ikimuonyesha alikuwa akimpiga mmoja wa wagombea wenzake ambaye alirekodi mazungumzo ya Ndugai wakati akiomba kura.

Wanavyomzungumzia

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Paul Loisulie alisema uamuzi wa Ndugai ni wa kupongezwa, kwani ameona mbali kufikiri namna gani anaweza kupisha damu mpya kwenda kumuongoza na yeye.

Mbunge wa zamani wa Kavuu, Dk Pudenciana Kikwembe alisema uamuzi wa Ndugai ni sahihi na unapaswa kuigwa na wanasiasa wengine.

Dk Kikwembe alisema kitendo cha kuamua mapema kinamfanya ajenge heshima kwa kila mtu na ndani ya chama chake1 ambacho kitafungua milango wakati ukifika.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema kanda ya kati, Aisha Luja alisema kauli kama hizo hutolewa mara nyingi na wanasaisa, lakini utekelezaji wake ni sifuri.

“Mara nyingi kauli kama hiyo mara nyingi hutolewa ili kupima upepo wa wapiga kura ambao mwisho wa siku husema kuwa wanamhitaji tena,” alisema.