NEC yazungumzia madai ya kura ‘feki’

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Jaji Semistocles Kaijage
Muktasari:
Baada ya baadhi ya wagombea ubunge wa vyama vya upinzani kudai kuwepo kwa kura feki katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Jaji Semistocles Kaijage amesema taarifa hizo hazijathibitishwa na kuwataka wananchi kuzipuuza.
Dar es Salaam. Baada ya baadhi ya wagombea ubunge wa vyama vya upinzani kudai kuwepo kwa kura feki katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage amesema taarifa hizo hazijathibitishwa na kuwataka wananchi kuzipuuza.
Baadhi ya wagombea waliodai kushuhudia kura feki ni Halima Mdee (Kawe), Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na baadhi ya wagombea wa majimbo ya Mkoa wa Tanga.
Akizungumza leo Jumatano Oktoba 28, 2020, Jaji Kaijage amesema, “kuna taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii kuhusu kuwepo kwa masanduku ya kura feki katika majimbo ya Kawe (Dar es Salaam), Pangani (Tanga) na Buhigwe (Kigoma). Taarifa za madai hayo za jumla ambazo sio rasmi hayajathibitishwa na hayaelezi ni vituo vipi vinahusika na matukio hayo.”
“Hivyo hivyo taarifa za madai hayo hazijawasilishwa rasmi kwenye tume ya taifa ya uchaguzi. Tume inawasihi wananchi kupuuza taarifa hizo ambazo siyo rasmi hazijathibitishwa.”