Necta yapanda miti kuongeza uzalishaji wa karatasi

Mufindi. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), linatarajia kupata miti 3,000 katika Kijiji cha Ikongosi, Shule ya Sekondari Mufindi na ya Msingi Mtilii, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ili kutunza mazingira na kuimarisha ulinzi kwa wanafunzi na walimu.

Miti hiyo inapandwa ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa baraza hilo mwaka 1973 na lengo ni kuhakikisha kunakuwa na karatasi za kutosha kwani mitihani inahitaji karatasi.

Akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mufindi wakati wa uzinduzi wa shughuli hiyo mapema wiki hii, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed amesema sababu za kupanda miti hiyo shuleni ni kurahisisha ustawi wa ulinzi kutoka kwa wanafunzi kwani baraza ndio miongoni mwa watumiaji wakubwa wa karatasi hizo.

"Ukipita kila nyumba huwezi kutembea nyumba moja hadi ya pili bila kukuta huduma ya Necta, kila nyumba inamtoto anasoma ama sekondari au shule ya msingi, amepita na amehudumiwa na baraza la mitihani," amesema Dk Mohamed.

“Kwa miaka mitano iliyopita, kuanzia mwaka 2018 hadi 2023, zaidi ya watahiniwa milioni 24 walisajiliwa kufanya mitihani mbalimbali. Watahiniwa hawa kama ni darasa la saba, mmoja anafanya mtihani kwa masomo sita na kila mtihani unakuwa na karatasi ngapi, karatasi za majibu ngapi, ukijumuisha utaona tuna mahitaji makubwa ya karatasi,” alisema

Alisema baraza linatambua umuhimu wa upandaji miti pamoja na utunzaji wa mazingira ndiyo maana wameamua kufanya shughuli hiyo huku akiwasisitiza wadau mbalimbali kujitokeza kushiriki.

Dk Mohamed amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuangalia namna nzuri ambayo wataona ni lazima wafanyie mabadiliko ya teknolojia ili waweze kujipanga miaka 50 ijayo iweze kuwa ya tofauti.

Alisema takwimu kidunia zinaonesha matumizi ya karatasi kwa miaka 40 iliyopita yameongezaka kwa zaidi ya asilimia 400. Ni muhimu kasi ya upandaji miti ikaongezwa kwani wakati miti bilioni 15 inakatwa kila mwaka kwa matumizi mbalimbali duniani, ni miti bilioni 1.9 ndiyo inayopandwa kwa mwaka.

Ofisa Elimu Mkoa wa Iringa,  Maria Lyimo  alizitaka  shule za sekondari  na msingi mkoani humo kupanda miti na kuitunza ikiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 50  ya baraza hilo.

“Tunapenda kukushukuru kwa kazi kubwa ambayo umeifanya katika shule zetu kugawa miti na kupanda ambayo itakuwa ni alama tosha kwa vizazi vijavyo kuwa Necta wakati wanaanzisha  miaka 50 walichagua shule hizo na kupanada miti ambayo ni ukumbusho mkubwa kwao,” amesema Lyimo.

Ofisa Misitu Mkuu wa Nyanda za Juu Kusini, Haruna Luganga ameishukuru Necta kwa kuwaunga mkono katika upandaji wa miti huku akiahidi kutoa ushauri wa kitaalumu ya namna ya upandaji wa miti hiyo ili iwe kielelezo kwa sehemu nyingine.

“Shughuli hii ikifanyika katika maeneo mengine ya ukanda huu kutatoa ushirikiano wa kutosha kuanzia utoaji wa miche utaalum wa namna ya uchimbaji wa mashimo kwa ajili ya kupanda na kutunza miti hiyo kwa sababu tumerithi basi nasi tuwarithishe,” amesema Luganga.

Mkurugenzi wa Halmashuri ya Wilaya ya Mufindi, Charles Fusi alitoa shukurani kwa wizara ya elimu kupitia Necta kwa kuchagua Wilaya ya Mufindi kuwa kitovu cha maadhimisho hayo, huku akiahidi kuhamasisha upandaji huo katika shule za halmashauri hiyo.

"Nishukuru baraza la Mitihani Tanzania kwa kuchagua Halmashauri ya Wilaya Mufindi kufanyika maadhimisho haya lakini ninaahidi kuhamasisha upandaji wa miti katika kila shule kwa halmshauri hiyo,” amesema.