NEMC yabaini kushamiri gereji bubu, kelele za muziki

Muktasari:

  • Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilianzishwa kwa Sheria ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira Namba 19 ya mwaka 1983 kama chombo cha kuishauri Serikali juu ya masuala ya utunzaji wa mazingira.

Dodoma. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limepokea malalamiko 369 ya wananchi kuhusu  uchafuzi  na uharibifu wa mazingira ikiwemo kelele za muziki kwenye nyumba za starehe huku wakibaini kushamiri kwa gereji bubu katika maeneo ya makazi.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa, Machi 3, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samweli Gwamaka wakati akieleza mafanikio ya baraza hilo katika kipindi ya miaka miwili ya utawala wa Serikali ya awamu ya sita kwa waandishi wa habari.

Kauli ya Mkurugenzi imekuja chache tangu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo alipotangaza hadharani baadhi ya kumbi za starehe na vilabu vya pombe kuwa wamezidisha kelele.

Dk Gwamaka amesema katika kipindi cha Julai hadi Februari 2022 wamepokea malalamiko hayo kuhusu kuvuja kwa mafuta kutoka kwenye mabomba ya mafuta, kuchoma taka hatarishi chini ya kiwango kinachotakiwa kisheria na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Malalamiko mengine ni utiririshaji wa maji taka, uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za viwandani, kelele za muziki, kushamiri kwa gereji bubu maeneo ya makazi, kushamiri kwa vituo vya mafuta katikati ya makazi na matumizi ya mifuko ya plastiki iliyokatazwa.

"Tunakabiliana na changamoto hizi kwa kutoa elimu kwa wananchi na tumeanzisha kanda tisa nchi nzima zenye wataalamu wa mazingira wanaoshughulikia changamoto hizo," amesema Dk Gwamaka.

Mkurugenzi amesema baraza linafanya tathmini zenye kulenga utoaji wa masuluhisho ya changamoto za mazingira, kufuatilia na kutathmini mifumo ya ikolojia.

Hata hivyo amesema wamejitahidi kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu kwa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi kwa kuweka utaratibu wa kufanya usafi kila siku ya Jumamosi.

Kuhusu changamoto ya uwekezaji kwenye maeneo yasiyo rasmi, amesema wamekutana na tatizo la Ujenzi wa Viwanda katika maeneo ya makazi ya watu ambalo ni tatizo.