Ni mwendo wa juisi ya tangawizi, kujifukiza

Ni mwendo wa juisi ya tangawizi, kujifukiza

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona huku akiwatoa hofu kuwa nchi ipo salama.

Dodoma. Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona huku akiwatoa hofu kuwa nchi ipo salama.

Kauli ya Dk Gwajima imekuja siku moja baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kuambukizwa virusi vya corona.

Juzi, chama cha ACT-Wazalendo kilitoa taarifa kuwa mwenyekiti wake, Maalim Seif anaumwa corona na alikuwa amelazwa hospitalini mjini Unguja.

Taarifa iliyotolewa na katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu ilieleleza kuwa kiongozi huyo, mke wake na wasaidizi wake nao walikuwa wanaumwa ugonjwa huo na Maalim Seif mwenyewe akaliambia gazeti hili kuwa mkewe alikuwa ametengwa.

Ni kipindi ambacho Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT), Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wametoa taarifa ya kuwataka waumini wao kujihadhari na magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Dk Gwajima aliwakumbusha watu kuchukua tahadhari ingawa alisisitiza hakuna maambukizo ya corona nchini.

Dk Gwajima alisema ugonjwa huo upo katika nchi jirani hivyo ni lazima Watanzania wachukue tahadhari zote zinazotakiwa kujikinga.

Tahadhari zinazotakiwa kuzingatiwa alisema ni elimu inayotolewa na wataalamu wa afya ikiwamo kuimarisha usafi, kujifukiza, kufanya mazoezi, kula lishe bora, kunywa maji mengi na matumizi ya tiba asili.

“Serikali itaendelea kuchukua tahadhari zote za ufuatiliaji na mwenendo wa magonjwa kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote na kuendelea kuelimisha wananchi juu ya hatua za kuchukua.

“Katika hili niwaelekeze waganga wakuu wa mikoa na wilaya, na maofisa mazingira kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti na kinga ya magonjwa kwa kushirikiana na wananchi ili kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza,” alisema.

Alisema wizara kwa kushirikiana na mkemia mkuu wa Serikali pamoja na Baraza la Tiba Asili wamesajili dawa asili ikiwamo covidol inayowasaidia watu wengi.

Kuhusu chanjo ya corona, alisema wizara haina mpango wa kuipokea. Alisema Serikali inazo taratibu za kufanya inapotaka kupokea bidhaa ya afya.

Aliliagiza Baraza la Tiba Asili nchini kutoa orodha ya dawa zote zilizopitia utaratibu wa uchunguzi wa kimaabara ya mkemia mkuu wa Serikali na kuonekana salama kwa matumizi.

Alisema Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa dawa nyingi zinazotolewa hopitalini zinatoka kwenye miti ya mkwinini ambayo hapa Tanzania inastawi wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Kwa upande wake, naibu waziri wa wizara hiyo, Dk Godwin Mollel alisema kwa miaka yote magonjwa ya kubanwa na kifua hulipuka kati ya Oktoba hadi Mei kutokana na hali ya hewa hivyo madaktari wanatakiwa kuwapima zaidi mgonjwa na si kusema ni corona.

“Kuna mheshimiwa mmoja alibanwa kifua, kufika hospitali akaambiwa ana corona nikamwambia nakuja kukuangalia akanisisitza usije, nina corona. Nilipofika akaniambia nimeshapewa dawa za corona. Nikaelekeza vipimo akakutwa presha ipo juu, walipotibu presha, kifua kikaachia,” alisema.

Kuthibitisha umuhimu wa kulinda afya, waziri, naibu wake pamoja na maofisa wengine wa Serikali walitengeneza juisi ya tangawizi na kuchanganya na matuda kisha kunywa huku wakisisitiza umuhimu wa kupiga nyungu.