Ni ukatili aisee, watoto wamzika baba yao mzazi akiwa hai

What you need to know:

  • Mzee Florence Komba (78), mkazi wa Kijiji cha Mahanje katika Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma, amezikwa akiwa hai kwa tuhuma kwamba amemuua mwanaye Severine Komba (34) kishirikina.



Madaba. Mzee Florence Komba (70), mkazi wa Kijiji cha Mahanje katika Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma, amezikwa akiwa hai kwa tuhuma kwamba amemuua mwanaye Severine Komba (34) kishirikina.

Tayari mzee huyo amefariki dunia baada ya watoto wake wawili kushirikiana na baadhi ya vijana wa kijijini hapo kumzika kwenye kabuli lililoandaliwa kwa ajili ya maziko ya Severine.

Akisimulia mkasa wa Severine uliosababisha mauaji hayo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mahanje, Jabiri Fussi alisema ulitokea Agosti 11 naye alipewa taarifa na wasamaria wema kuwa mtoto wa Komba amejifungia ndani na hajaonekana kwa siku mbili na si kawaida yake.

Baada ya kupokea taarifa hizo, alisema alienda nyumbani kwa marehemu na kukuta mlango umefungwa kwa ndani hivyo akawasiliana na mkuu wa kituo cha polisi aliyempa ridhaa ya kuuvunja mlango huo.

“Baada ya kuvunja mlango tulimkuta mtu (Severine Komba) amefariki dunia, tulikaa na familia kufahamu kama kuna mashaka yoyote juu ya kifo hicho, walijibu hakuna mwenye mashaka kwakuwa marehemu alikuwa anaumwa kwa muda mrefu na alikuwa anaishi peke yake. hakua na mke wala watoto,” alisema Fussi.

Kutokana na kauli ya wanafamilia hao, Fussi alisema aliruhusu maziko yaendeleea na wanafamilia walikubaliana yafanyike Agosti 12, saa tatu asubuhi hivyo yeye akaondoka kwenda kushiriki ziara ya Mbunge wa Madaba, Dk Joseph Mhagama kukagua miradi ya maendeleo jimboni.

Akiwa kwenye ziara hiyo, alisema alipigiwa simu na kujulishwa kuwa maziko ya Severine aliyoruhusu yafanyike watoto wa familia hiyo wamemzika baba yao mzazi wakimtuhumu kuhusika na kifo cha mwanawe huyo kuwa ndiye aliyemuua kwa imani za kishirikina.

“Aliniambia walimpiga sana na kisha wakamchukua na kwenda kumzika kwenye kaburi lililochimbwa kwa ajili ya kumzika Severine,” alisimulia Fussi na kuongeza:

“Baada ya kupata taarifa niliwasiliana na polisi waliofika bila kuchelewa. Walienda hadi makaburini, wakaufukua mwili wa mzee huyo na kuutoa ili taratibu zaidi za kisheria zifanyike na baada ya kukamilika taratibu hizo, ndipo tuliuhifadhi upya mwili huo.”

Mtendaji huyo alisema inadaiwa wakati watoto hao na baadhi ya watu wengine wakitekeleza kitendo hicho Agosti 12, maiti ya Severine ilikuw aimeachwa ndani na ilizikwa juzi.


Mkuu wa wilaya alaani

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisema alipopata taarifa hizo aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama hadi eneo la tukio kushuhudia kilichotokea ambako alikemea kitendo hicho cha kikatili kwamba hakipaswi kufumbiwa macho na lazima hatua za kisheria zichukue mkondo wake.

Alisema unyama huo hauwezi kuvumiliwa na alishangaaa kuona wanaotuhumiwa ni watoto waliozaliwa na mzee Komba.

“Binafsi nalaani tukio hili la kinyama lililotekelezwa na watoto wake, hii haikubaliki. Naagiza wote waliohusika kufanya kitendo hiki wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe, sitaki tena tukio kama hili lijirudie,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Alisema Kijiji cha Mahanje kimekuwa na matukio mengi ya ajabu akieleza kuwa miezi miwili iliyopita, alipata taarifa za vijana kutaka kumuua mzazi wao wakimtuhumu kwa imani za kishirikiana tukio alilosema lilidhibitiwa na Jeshi la Polisi waliowahi eneo husika.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaonya wananchi aliodai wako mstari wa mbele kuhamasisha vurugu kuacha vitendo hivyo mara moja kwa sababu Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali pale watakapobainika.


Ndugu wasimulia

Stephano Mapunda, mmoja wa ndugu wa familia ya mzee Komba anayeishi Mahanje ambaye ni diwani wa kata hiyo aliliambia Mwananchi kuwa ameumizwa na tukio hilo kwa sababu kabla ya Komba kufikwa na mauti, watoto wake walimchukua na pikipiki na kumpeleka makaburini kwa ajili ya kumwonyesha eneo ambalo lingechimbwa kaburi la kumzika mtoto wake Severine.

“Kumbe alikuwa anajiandalia mwenyewe kaburi bila kujua,” alisema Mapunda kwa masikitiko.

Mapunda alisema Komba alishawahi kuwa mhasibu wa kijiji kwa miaka mingi na baadaye akawa mkulima mkubwa na hakuwahi kusikia akituhumiwa kwa uchawi kutoka kwa mtu yeyote na hii ni mara ya kwanza anasikia kuwa ni tuhuma zilizoibuliwa na watoto wake mwenyewe.

“Nasikitika sana, hili ni tukio la pili na yote huwa yanaanzishwa na vijana wa marehemu. Nawaomba vijana waache kushiriki vurugu na mauaji kama kuna kitu hakipo sawa wazungumze na viongozi wa Serikali na si kuua watu, mke wa marehemu alishafariki siku nyingi hivyo alikuwa akiishi peke yake,” alisema Mapunda.


Jirani asimulia

Neema Mahundi, jirani wa marehemu Komba alisema “nimeumizwa sana na kifo cha Mzee Komba, ni cha kikatili sana. Hili jambo ni baya sana, naomba wote waliohusika wachukuliwe hatua ili kukomesha vitendo kama hivi hapa kijijini kwetu, vijana wengi wanaamini sana ushirikina jambo ambalo siyo zuri.”

Neema alisema tukio hilo limewasikitisha watu wengi kijijini hapo kwamba Komba alikuwa mzee mwenye heshima yake kijijini hapo na hakuwa na ugomvi na mtu yeyote ila inashangaza kuona watoto wake wa kuwazaa ndio wameamua kumvunjia heshima na kumsababisha kifo.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.