Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nida kurekebisha vitambulisho vyenye hitilafu

Muktasari:

  • Hitilafu zitakazofanyiwa kazi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ni pamoja taarifa zilizochapwa mbele au nyuma ya vitambulisho, kufutika majina, namba ya kitambulisho au tarehe ya kuzaliwa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imewaelekeza wananchi ambao vitambulisho vyao vina hitilafu kuvikusanya kwenye ofisi za Serikali walipovichukua ili wapatiwe vilivyorekebishwa.

Nida imetoa maelekezo hayo katika taarifa yake jana Jumamosi Julai 20 2024 baada ya wananchi kulalamikia hitilafu kwenye  vitambulisho.

Hitilafu hizo ni taarifa zilizochapwa mbele au nyuma ya vitambulisho, kufutika majina, namba ya kitambulisho au tarehe ya kuzaliwa.

Katika kushughulikia tatizo hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho vya Nida,  Edson Guyaye amesema mamlaka hiyo imetoa maelekezo kwa maofisa wake wa usajili katika wilaya zote kukusanya vitambulisho vyenye changamoto hiyo.

“Tunatoa rai pia kwa watendaji wa Serikali za mitaa, kata, vijiji, vitongoji na shehia kwa upande wa Zanzibar, kuvikusanya vitambulisho hivyo na kuvirejesha kwenye ofisi za Nida wilayani ili vichapishwe upya bila malipo kwa mwananchi,” amesema Guyaye.

Amesema kumekuwa na upotoshaji mkubwa kuhusu ubora wa vitambulisho vya Taifa kutokana na changamoto zilizojitokeza, huku akisisitiza kuwa, vitambulisho vinavyotolewa na mamlaka hiyo vinakidhi viwango vya ubora wa kimataifa.

“Kwa sasa wataalamu wetu wanaendelea na uchunguzi wa kubaini chanzo cha tatizo hilo kama ni mashine, wino au kadi ghafi zilizotumika na kadhalika. Hii itatuwezesha kufidia kadi hizo kama ilivyoelezwa kwenye mkataba na mkandarasi bila Serikali kuingia gharama ya ziada,” amesema Guyaye.

Amesema hitilafu ndogondogo ni jambo la kawaida kutokea katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa duniani huku akieleza kuwa, kampuni kubwa za uzalishaji kama magari na simu pia hupata changamoto.

Mkurugenzi huyo amesema takwimu za mamlaka hiyo zinaonyesha kuwa vitambulisho vyenye hitilafu ni 21,224 sawa na asilimia 0.09 ya vitambulisho 21,322,098 vilivyozalishwa.

Guyaye amesema Serikali ya Awamu ya Sita ilitoa Sh42.5 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa malighafi kuhakikisha wananchi wanaondokana na changamoto ya kutokuwa na vitambulisho vya Taifa.

“Fedha hizo ziliiwezesha Nida kupanga na kutekeleza mkakati mkubwa wa uzalishaji vitambulisho  uliokwenda sambamba na usambazaji na ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa umma,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema jumla ya vitambulisho milioni 21 vimezalishwa kwa wananchi wenye sifa na kupelekwa katika ngazi ya mtaa, vijiji, kata na shehia huku jumla ya vitambulisho milioni 19 zikichukuliwa na wahusika.

Juzi, wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Songwe, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Serikali imezindua mkakati maalumu wa utoaji vitambulisho kwa wananchi waishio mipakani na mambo yatakuwa mazuri yakifanyika mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa Nida.

“Tumeanza kuzitatua changamoto hizo hatua kwa hatua. Mtakumbuka Rais alitupa ushauri wa kuwa na namba moja ya utambulisho wa Mtanzania. Mambo haya ni muhimu kuyafanyia utafiti kuangalia muundo na utendaji kazi wa Nida kwa jumla wake.

“Mambo haya yanahitaji mabadiliko ya sheria. Kamati iliyokuwa kazini, imemaliza kazi yake. Tunataka chombo hiki kifanye kazi yake kwa ufanisi ili kupunguza malalamiko ya wananchi,” amesema Waziri Masauni.