Nida yatoa utaratibu mpya kupata namba ya utambulisho wa taifa

Muktasari:

Pamoja na namba za utambulisho wa Taifa (NIN) kukutambulisha, pia zinatumika katika usajili wa alama za vidole za laini za simu unaoendelea Tanzania hadi Desemba 2019 ambapo laini ambazo hazitasajiliwa zitasitishiwa huduma.

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wengi wakiwa na changamoto ya kupata namba ya utambulisho wa Taifa (NIN), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imewarahisishia kwa kuweka utaratibu wa kuipata kwa njia ya mtandao.

Taarifa iliyotolewa na Nida jana Jumatano Septemba 25, 2019 kupitia kitengo cha mawasiliano na hifadhi hati ilisema namba hiyo sasa imeanza kutolewa kupitia tovuti ya mamlaka hiyo kwa muombaji kutembelea https://services.nida.go.tz/nidpotal/get_nin.aspx.

Taarifa ya Nida ilibainisha kwamba huduma hiyo itawarahisishia waliojisajili kuomba vitambulisho vya Taifa kupata NIN bila kwenda ofisi za mamlaka hiyo.

Hatua za kufuta kupata namba ya NIN

Tembelea tovuti ya NIDA ya www.nida.go.tz

Bonyeza kitambulisho cha Taifa

Fahamu namba ya utambulisho wa Taifa

Andika jina lako la kwanza, jina la ukoo, tarehe ya kuzaliwa, jina la kwanza la mama na jina la mwisho la mama

 

Bonyeza Tafuta

Aidha Nida imefafanua kuwa namba za NIN pia zimepelekwa ofisi za kata ili kuwapunguzia waombaji adha ya kufuata namba hizo ofisi za Nida za wilaya.

"Waombaji pia wanaweza kupata NIN kwa kupiga simu au kutuma ujumbe kwenye kituo cha huduma kwa mteja," ilieleza taarifa hiyo.