NIMR yatengeneza dawa nane za asili
Muktasari:
- Dawa zilizotengenezwa ni pamoja na Warbugistat inayotibu magonjwa nyemelezi, Nimrevit ambayo ni kinywaji lishe, Nimregenin kwa ajili ya tezi dume na Tangesha kwa ajili ya seli mundu, Ipo Persivin inayoondoa uvimbe wa saratani, TMS 2001 kwa ajili ya ugonjwa wa malaria na Nimrcaf.
Dar es Salaam. Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kupitia kiwanda chake cha kutengeneza dawa za asili cha Mabibo jijini hapa, kimetengeneza dawa nane zitokanazo na miti kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali.
Akizungumza leo Septemba 14 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi ilipotembelea kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud amesema tangu kituo hicho kilipoanzishwa mwaka 2021 kimekuwa kikifanya utafiti wa dawa za asili.
“Mpaka sasa kituo kina jumla ya dawa za toba asili nane ambazo zipo katika majaribio kwa binadamu. Ipo Warbugistat inayotibu magonjwa nyemelezi, Nimrevit ambayo ni kinywaji lishe kwa ajili ya kuimarisha afya, Nimregenin kwa ajili ya tezi dume na Tangesha kwa ajili ya seli mundu.
“Ipo Persivin inayotumika kuondosha uvimbe hasa kwa wagonjwa wa saratani, TMS 2001 kwa ajili ya ugonjwa wa malaria na Nimrcaf inayosaidia jamii kupambana na Uviko-19, hivyo ipo katika utafiti zaidi ili isaidie jamii kutibu magonjwa ya vvifua na kuimarisha kinga,” alisema.
Akizungumzia dawa ya Nimrevit inavyofanya kazi, mfamasia Abel Mdemu amesema inasaidia kuondoa sumu mwilini na kuuwezesha mwili kupambana na magonjwa.
“Wakati mchakato wa oxidation (uongezwaji wa hewa ya oksijeni) unasaidia mwili kujilinda na magonjwa. Mwili wako umeumbwa na uwezo wa kujirekebisha wenyewe, ila kuna wakati huo uwezo unapotea. Sasa kuna vyakula unatakiwa utumie ili kurejesha na ndio tunashauri utumie hii dawa,” amesema.
Akizugumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Faustine Ndugulile ameitaka Wizara ya Afya kuharakisha usajili wa dawa za asili.
“Tulikutana na Wizara ya Afya na Baraza la Tiba asili na Tiba Mbadala na katika wasilisho lao walitujulisha kuwa wamesajili zaidi ya wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala 20,000.
“Lakini dawa ambazo zimesajiliwa hazifiki tano nchi nzima. Maana yake ni kwamba tuna wataalamu wengi wa tiba za asili na tiba mbadala wanaofanya kazi zao bila dawa zao kutambuliwa na Serikali.
Alisema kutosajiliwa kwa dawa hizo kunaleta hatari ya kuongezeka kwa magonjwa yakiwamo ya figo.
“Hapa ni suala zima la uratibu, ukiangalia ndani ya Wizara ya Afya, kuna taasisi nne zinazohusika na masuala ya tiba za asili. Kuna Baraza lenyewe, kuna NIMR, kuna Mkemia Mkuu wa Serikali na kuna Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),” amesema.
Alitaja pia changamoto ya gharama kubwa za usajili wa dawa hizo, akisema zinaawafanya wataalamu hao kukwepa usajili.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati, Stanslaus Nyongo akiitaka Serikali kuangalia sheria za matumizi ya dawa za asili.
“Zile sheria za tiba asilia, imefika wakati matangazo yamekuwa mengi sana. Ukipita barabarani watu wanatangaza, mtu anatibu magonjwa mbalimbali.
“Mwone namna ya kukaa na Baraza la Tiba Asiliana na Tiba Mbadala mwone namna ya kukaa na kuhakikisha sheria zinazingatiwa,” alisema.