Nondo aruka kiunzi kimoja, abakiza vitatu

Muktasari:
Jana Jumatatu Novemba 5, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemwachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo baada ya kushindwa kumtia hatiani
Iringa/Dar. Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo ameruka kiunzi cha kwanza kati ya vitatu katika masaibu aliyokumbana nayo karibuni.
Kiunzi hicho cha kwanza alikiruka jana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa kumwachia huru baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka mawili yaliyosababisha afikishwe mahakamani hapo.
Viunzi alivyovibakiza ni kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitampokea baada ya kumsimamisha siku 224 zilizopita na kama Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu itaendelea kumpa mkopo. Kingine ni suala lake la uraia unaoendelea kuchunguzwa na Idara ya Uhamiaji.
Nondo alisimamishwa chuo Machi 26, baada ya kufikishwa mahakamani na Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye akizungumza na Mwananchi Machi 27, alisema walifanya hivyo kwa mujibu na taratibu za chuo.
Profesa Anangisye alisema mwanafunzi anapokuwa amepandishwa kizimbani na akawa na kesi ya kujibu, husimamishwa na akishamaliza kesi yake anarejea kuendelea na masomo.
Hata hivyo, naibu makamu mkuu wa chuo cha UDSM-Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa akizungumza na Mwananchi jana baada ya hukumu kutoka alisema hawajapata taarifa rasmi ya Nondo kuachiwa huru.
“Bado tunaona taarifa hizo katika mitandao ya kijamii, hatujapata taarifa rasmi, tukipata tutaweza kuona taratibu zingine zinafuatwa sasa,” alisema Profesa Rutinwa.
Nondo aliyesimamishwa akiwa mwaka wa tatu akisoma Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma alipoulizwa utaratibu wa kurejea chuoni alisema, “Sasa kesi imeisha nitarudi chuo kama barua ilivyojieleza. Ila kuna haja sasa ya kuanza kuangalia sheria hizi tulizonazo vyuoni kama zipo sawa.
“Unapomsimamisha mwanafunzi kwa tafsiri ndogo, inakuwa tayari umemhukumu kuwa ni mkosaji wakati chombo chenye dhamana ya kuhukumu ni mahakamani. Kuna haja ya kuanza kuangalia ‘fairness’ ya hizi sheria zetu, ili zisiathiri wengine huko mbele,” alisema Nondo.
Alipoulizwa anatarajia kurejea lini chuoni alisema, “Sitarudia mwaka, nilibakiza muhula mmoja wa mwisho hivyo natarajia kurudi Machi mwakani.”
Kuhusu suala la mkopo kama alikuwa anapata alisema, “Ndiyo nilikuwa na mkopo ila ulizuiwa.”
Alipoulizwa kama ana matumaini ya kupata mkopo atakaporejea chuoni, alisema, “Nina haki hiyo ya kuendelea kupewa mkopo labda kuwe na mambo mengine kwa kweli.”
Alipoulizwa kuhusu kuchunguzwa uraia wake alisema, “Hakika hilo sina shaka nalo, sababu wamesema bado wanaendelea na upelelezi.”
Nondo alifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Machi 21, akikabiliwa na makosa mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo kwamba “nipo hatarini” na kuzisambaza mtandaoni.
Kosa la pili, lilikuwa ni kutoa taarifa za uongo kwa askari Polisi, Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto mjini Mafinga.
Jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Liad Chamshana akitoa hukumu hiyo alisema katika kosa la kwanza, upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha uongo wa maneno ya mshtakiwa, maana ya maneno ‘nipo hatarini’ na nani aliyesambaza maneno hayo.
Hakimu Chamshana alisema shahidi wa kwanza hadi wa sita hawakuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya kosa hilo na badala yake walitumia hisia na mashaka, jambo lililowafanya washindwe kuithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka kwamba mshatakiwa ndiye aliyeandika maneno hayo ya uongo.
Kwa msingi huo, Chamshana alisema Mahakama imeyaangalia maneno hayo ‘nipo hatarini’ na kujiridhisha kwamba yana maana pana ambayo ni ngumu kuitumia kumuadhibu mshtakiwa huyo.
Alisema upande wa Jamhuri umeshindwa pia kuthibitisha kama Nondo ndiye aliyesambaza maneno hayo, kwa sababu ushahidi wao unaonyesha yalisambazwa na shahidi wao wa tatu ambaye ni mwanafunzi anayesoma pamoja na mshtakiwa huyo UDSM.
Katika kosa la pili, Chamshana alisema upande wa Jamhuri ulishindwa pia kuthibitisha kosa la mshtakiwa huyo aliyekwenda katika Kituo cha Polisi cha Mafinga kama mlalamikaji kabla malalamiko yake hayajageuzwa na kuwa mashtaka yake.
“Upande wa Jamhuri na utetezi wote wanakubali kwamba Machi 7, 2018 mshtakiwa alikuwa Mafinga na alikwenda kituo cha Polisi kutoa malalamiko yake,” alisema.
Alisema cha kushangaza, mashahidi wote saba wa upande wa Jamhuri walishindwa kutoa ushahidi unaoonyesha namna mshtakiwa huyo alivyofika Mafinga na ule unaoonyesha kabla ya kufika Mafinga alikuwa wapi ili kuthibitisha kama alitekwa au alijiteka.
Hakimu Chamshana alishangaa kwa nini vyombo vilivyofanya upelelezi (polisi) dhidi yake viliacha majukumu yao ya kipolisi ili viweze kuthibitisha madai hayo na badala yake vikamchukulia mshtakiwa huyo kama mhalifu.
“Kwa msingi huo Mahakama imeshindwa kuyaamini mashtaka yaliyotolewa na upande wa Jamhuri na hivyo inamuachia huru mwanafunzi huyu,” alisema na kuongeza kwamba upande wa mashtaka unaweza kukata rufaa.
Nje ya Mahakama
Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa aliishukuru Mahakama kwa kutenda haki akisema, “Haki imetolewa kwa mujibu wa sheria na ushahidi na vielelezo vilivyofikishwa mahakamani.”
Ole Ngurumwa, ambaye taasisi yake ndiyo iliyotoa mawakili wa kumtetea mwanafunzi huyo, alisema hatua inayofuata baada ya kuachiwa huru ni kuhakikisha Nondo anapata haki yake ya kuendelea na masomo kutokana na uongozi wa chuo chake kumsimamisha.
Wakili wake, Jebra Kambole alisema Jamhuri ilishindwa kuonyesha pasipo shaka kwamba mteja wake alitenda makosa hayo.