Nyara za Serikali zakamatwa hifadhi ya Isawima

Muktasari:
Watu wanaodhaniwa kuwa ni majangili wametupa nyara za Serikali ikiwemo ngozi ya Chui, Swala na Statunga wakati wakikikimbia kukwepa mkono wa sheria.
Tabora. Nyara za Serikali ikiwemo ngozi ya chui, ya swala na statunga zimekamatwa kwenye hifadhi ya Isawima mkoani Tabora baada ya kutupwa na watu wanaodhaniwa majangili wakati wakikimbia kukwepa askari wa wanyamapori.
Katibu wa hifadhi ya Isawima, Hamis Katabanya amesema nyara hizo zikiwemo pembe za swala zilikuwa mikononi mwa watu wanaodhaniwa ni majangili ambao walizitupa kutokana na kuwaona askari waliokuwa wakifanya doria eneo hilo.
"Nyara hizi zimekamatwa kutokana na doria inayofanywa na hifadhi hii kwa kushirikiana na kamati ya Usalama ya Wilaya na Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori (Tawa) kanda ya magharibi,"amesema
Katabanya ameeleza kuwa eneo hilo ambalo linahifadhiwa tangu 2007 kwa lengo la kutunza mazingira na kunufaika na rasilimali zilizopo wakiwemo wanyamapori kuwa limekuwa likivamiwa mara kwa mara na baadhi ya watu wenye mifugo kwa lengo la kutafuta malisho na maji.
Amebainisha kuwa baadhi ya wafugaji pamoja na kuomba kujipatia maji na malisho, wamekuwa wakivamia eneo hilo na kufanya vitendo vya ujangili ambavyo havikubaliki kwani ni kinyume cha sheria na lengo la kuanzishwa hifadhi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Hifadhi ya Isawima, Morrice Gahame amewataka wafugaji wanaopanga kulisha mifugo yao kwenye hifadhi ya Isawima kutambua kuwa ni makosa na kuwashauri kuwa na mifugo ambayo watamudu kuitunza pasipo kuwaza kulisha kwenye maeneo ya hifadhi.
Hifadhi ya Isawima ilianzishwa na vijiji 11 vilivyoamua kutoa baadhi ya maeneo yao kwa lengo la kutunza mazingira na kunufaika na rasilimali zilizopo.