Nyerere alivyoiandaa CCM kwa vyama vingi-2
Muktasari:
Katika toleo lililopita tulianza kuangalia namna Baba wa Taifa, Julius Nyerere alivyokuwa na pande mbili katika suala la demokrasia, upande mmoja alionekana ni mkandamizaji na upande mwingine mchocheaji wa mabadiliko ya vyama vingi kutoka mfumo wa chama kimoja.
Katika toleo lililopita tulianza kuangalia namna Baba wa Taifa, Julius Nyerere alivyokuwa na pande mbili katika suala la demokrasia, upande mmoja alionekana ni mkandamizaji na upande mwingine mchocheaji wa mabadiliko ya vyama vingi kutoka mfumo wa chama kimoja.
Mwaka 1965 utawala wake ulifuta mfumo wa vyama vingi iliourithi kutoka kwa wakoloni, hata hivyo jicho la pili laweza kumuangalia Baba wa Taifa kama mwanasiasa aliyekubali kuwa siasa za chama kimoja zisingeweza kudumu.
Atakumbukwa kwa namna alivyoiandaa CCM kwa vyama vingi kupitia mikutano na hotuba mbalimbali. Hotuba ambayo ilipata umaarufu sana ni ile aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Februari, 1992 jijini Dar es Salam baada ya Tume ya Nyalali kuwasilisha ripoti ya maoni ya wananchi yaliyoonyesha kuwa asilimia 20 tu ndio walikuwa wakitaka vyama vingi.
“Mageuzi haya hayana budi kusimamiwa na kuongozwa na Chama cha Mapinduzi chenye umoja, nguvu na mshikamano. Ndugu wananchi, ndugu wajumbe, naomba mniamini katika hilo. Nalisema na kuliamini kwa dhati ya moyo wangu. Lakini naomba mniamini pia katika hili lifuatalo.
“Historia ni sehemu ya historia ya chama chetu na nchi yetu. Ni matokeo halali kabisa ya kuwa na chama kimoja chenye nguvu na kinachopendwa na wananchi kwa muda mrefu. Lakini sasa tunazungumzia uwezekano wa kuruhusu mfumo wa vyama vingi.
“Mimi sitashangaa hata kidogo ikiwa baada ya sheria kubadilika, baadhi ya wanachama wa CCM wataona kuwa mawazo yao hayawezi tena kuwa na manufaa au kueleweka kiasi cha kutosha ikiwa watabaki ndani ya CCM. Wakiamua kutoka katika CCM na kuanzisha chama kingine, kwa maoni yangu tutafanya makosa makubwa sana kuwaona kuwa ni wasaliti.
“Kama tutaanzisha utaratibu wa vyama vingi kwa moyo mmoja, basi tunataka vyama ambavyo vinaweza kuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuunda serikali ya nchi yetu.
“Halmashauri Kuu ya Taifa haituombi tutoe ruhusa ya kuanzisha utitiri wa vyama vya hovyo hovyo. Nani anavitaka? Nani anavitaka vyama vya utitiri? Vya hovyo hovyo! La sivyo baadhi ya wanachama wa CCM watasema ‘potelea mbali’, na wataanzisha chama au vyama na kukabili kutukanwa na wenzao watakaobaki ndani ya CCM.
“Matokeo ni kutukanana na tutakuwa tumeweka msingi wa vyama vya uhasama. Nani anataka vyama vya uhasama?
“Najua wapo watu wanaodhani kuwa vyama vya siasa ni vyama vya uhasama. Matumaini yangu ni kwamba watu hawa hawamo ndani ya CCM. Basi, tufanye kitendo ambacho kitawasaidia au kitatufanya sisi tusifanane nao.
“Leo tunajadiliana juu ya tofauti zetu ndani ya chama kimoja. Wakati mwingine kama nilivyosema tunazivungavunga tofauti zetu kwa sababu ya kuoneana haya. Lakini hatugombani na tofauti zetu zinabaki palepale.
“Kesho bila ya kubadili mawazo yetu na kwa kuamini kwa dhati kabisa kwamba tunaweza kuendeleza mawazo hayo vizuri zaidi. Tunaweza tukajikuta katika vyama viwili mbalimbali.
“Kwa nini tugombane! Na tutukanane! Ni kweli kwamba sasa tutalazimika kuzielewa tofauti zetu waziwazi zaidi na hadharani ili wananchi waweze kuzielewa. Hilo ni jambo la kawaida katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi. Lakini si sababu ya kutugombanisha.”
James Mbatia: Alikuwa baba wa demokrasia’
James Mbatia, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, anasema Mwalimu Nyerere alifanya kazi muhimu ya kufagia njia kwa ajili ya vyama vingi kurejeshwa.
“Kweli alikuwa ni baba wa demokrasia. Alitumia nguvu yake kuishawishi CCM kukubaliana na mfumo wa vyama vingi,” anasema Mbatia baada ya kuulizwa kama ushiriki wa Mwalimu katika mijadala ulisaidia.
“Aliiambia dunia mwelekeo ambao nchi ilikuwa inachukua. Wakati wa ripoti ya Tume ya Nyalali, alieleza umuhimu wa kuingia mfumo wa vyama vingi licha ya kuonekana kuwa ni asilimia 20 tu ndio waliotaka.
“Aliwaambia umuhimu wa kukubali vyama vingi wakati huo badala ya kusubiri idadi ifikie asilimia 80. Hapo alifanikiwa.”
Lakini Mbatia, ambaye ndio kwanza alikuwa anaingia katika siasa baada ya kukumbana na matatizo chuo kikuu, anasema hata hivyo Mwalimu Nyerere aliingiwa na wasiwasi wa nchi kuongozwa na chama kingine.
“Hakusimamia kuweka mifumo ya vyama vingi. Wengine waliokuja nyuma yetu kama Kenya, wametuacha mbali. Walitengeneza upya katiba wakafanya maridhiano, sisi bado tuko mbali sana,” anasema Mbatia.
“Akaacha kusimamia kupata katiba mpya. Akaacha kusimamia mali za umma zisichukuliwe na CCM ili vyama vyote vianze upya. Sheria ya uchaguzi inatakiwa iseme mshindi apate asilimia 50+. Kwa hiyo akaacha kuwa Baba wa Taifa akawa Baba wa CCM.”
‘Aliona kuna vyama mamluki’
Maoni ya Mbatia yanalingana kwa kiasi fulani na mwenyekiti wa Ada-Tadea, John Shibuda ambaye anasema Mwalimu Nyerere alilazimika kuelimisha umuhimu wa vyama vingi baada ya kuona sera ya kujisahihisha imefeli, ubinafsi wa wananchi wa Tanzania Bara dhidi ya Wazanzibari na pia kutaka kuwahi kuchukua hatua kabla ya wimbi la mageuzi lililokuwa linaendelea duniani kuikumba Tanzania.
“Tulishakuwa na mfumo wa vyama vingi wakati tunadai uhuru, lakini Mwalimu aliufuta baada ya kuona kuna vyama mamluki vilivyokuwa vinafadhiliwa na gavana kwa ajili ya kuvi-distabilise vyama makini,” anasema.
Alisema Bara kilikuwepo chama cha African Moslems, ambacho kilikuwa kimetengenezwa na gavana, wakati Zanzibar kulikuwa na chama cha Zanzibar Nationalist Party, akisema kilikuwa cha mamluki.
“Ili kuwe na mshikamano, alilazimika kufuta vyama vingi,” alisema.
Kwa mujibu wa Shibuda, baada ya kufuta Mwalimu alianzisha sera ya kujisahihisha ambayo ililenga kujikosa na kujiimarisha, lakini ikafeli kwa kuwa Wana-CCM waliendelea kuwa na umimi na hawakujisahihisha na ndipo Mwalimu alipokumbatia mageuzi ili yaiamshe CCM.
“Wimbi la mageuzi lilishaanza duniani, Mwalimu alitaka nchi iwahi kuchukua hatua kabla ya wimbi la mageuzi duniani kuifikia Tanzania,” alisema Shibuda, ambaye anaamini kuwa hadi leo kuna vyama mamluki vilivyosajiliwa kwa ajili ya “kuviyumbisha vyama makini kama Chadema”.
Pamoja na yote hayo, kulikuwa na kila haja ya Mwalimu Nyerere kushiriki katika mijadala ya vyama vingi ili kuwaaminisha wananchi kuwa muda ulikuwa umefika wa kujadili bila woga mawazo tofauti ya jinsi ya kuiendesha nchi.