Nyerere alivyoiandaa CCM kwa vyama vingi

Muktasari:

Julius Kambarage Nyerere anaweza kuzungumziwa na baadhi ya wanasiasa na watu wengine kama kiongozi aliyekandamiza demokrasia kutokana na uamuzi wa Serikali yake wa mwaka 1965 wa kufuta mfumo wa vyama vingi iliourithi kutoka kwa wakoloni.

Julius Kambarage Nyerere anaweza kuzungumziwa na baadhi ya wanasiasa na watu wengine kama kiongozi aliyekandamiza demokrasia kutokana na uamuzi wa Serikali yake wa mwaka 1965 wa kufuta mfumo wa vyama vingi iliourithi kutoka kwa wakoloni.

Zaidi ya kufuta demokrasia ya vyama vingi, wanasiasa walioonekana kuwa na mitazamo tofauti ya kisiasa na Serikali yake walikumbana na wakati mgumu katika kipindi chote ambacho nchi ilifuata siasa za chama kimoja, wakiwemo kama James Mapalala na Mwinyijuma Othman Upindo ambao walidai kurejeshwa kwa siasa za ushindani na kujikuta wakiwekwa kizuizini na baadaye uhamishoni ndani ya nchi kwa takriban miaka minne.

Uhuru wa maoni ulikuwa ndani ya chama kimoja Bara na Visiwani, yaani Tanu kwa upande wa Bara na ASP kwa upande wa Zanzibar na baadaye mwaka 1977 Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa na haki pekee ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lakini jicho la pili laweza kumuangalia Baba wa Taifa kama mwanasiasa aliyekubali kuwa siasa za chama kimoja zisingeweza kudumu katika dunia mpya iliyokumbwa na wimbi la mageuzi kuanzia barani Ulaya hadi Afrika.

Ukuta wa Berlin uliozitenganisha nchi za Ujerumani Mashariki na Magharibi uliangushwa mwaka 1989 baada ya serikali ya kikomunisti ya Ujerumani Mashariki kuachia ngazi na kumsha shangwe kwa wananchi wake ambao walikimbilia kwenye ukuta huo uliokuwa na urefu wa maili 28 na kuanza kuubomoa kwa mashoka na zana nyingine, ili kupata njia za kwenda Magharibi kuonana na wenzi wao.

Hiyo ilikuwa ni ishara ya anguko la siasa la nchi za Mashariki ambako hakukuwa na demokrasia ya uhuru wa mawazo iliyopo duniani sasa.

Anguko la pili lilisababishwa na mageuzi (perestroika) ndani ya Chama cha Kikomunisti cha Umoja wa Kisovieti (CPSU) na uwazi (grassnot) yaliyoanzishwa na katibu mkuu wa chama hicho, Mikhail Gobachev miaka ya themanini mwishoni na kuhitimika mwanzoni mwa miaka ya tisini wakati dola hilo la Kisovieti lilipoanguka na baadhi ya nchi kujitoa ndani ya Urusi.

Hiyo ilikuwa ishara tosha ya, kwanza, kumalizika kwa vita baridi iliyoigawanya dunia katika pande mbili, na pili ni kuanguka kwa dola la Urusi (sasa Russia). Au kwa maana nyingine ilikuwa ni ushindi wa demokrasia.

Wimbi la mageuzi likaanza kusambaa sehemu nyingine na hatimaye kufika Afrika ambako vyama vilivyoshiriki ukombozi na baadaye kuamua kufuata siasa za chama kimoja, vilijikuta katika wakati mgumu na baadaye kulazimika kurejesha siasa za vyama vingi, ikiwemo Zambia ambako Rais Kenneth Kaunda aliangushwa na chama cha upinzani mwaka 1991.

Wakati wimbi hilo likizidi kusambaa, Baba wa Taifa hakukaa kando na mijadala ya kuingiza siasa za ushindani. Kila alipopata nafasi ya kuzungumza, alijadili umuhimu wa kuwepo na mijadala ya dhati kabla ya kukubali au kukataa siasa za vyama vingi.

Kati ya kauli maarufu alizotoa Mwalimu Nyerere kuonyesha kuwa mabadiliko ni lazima ni ile aliyotoa katika mkutano mkuu maalumu wa CCM wa kumpitisha Benjamin Mkapa kuwa mgombea wa urais wa chama hicho mwaka 1995.

“Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyaona au wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM,” alisema Nyerere.

Pia kauli kwamba “CCM si mama yangu, ikiyumba naondoka” ilizidi kuonyesha kuwa kuondoka chama hicho tawala hakukuwa usaliti tena.

Alianza kuchangia mijadala hiyo mapema miaka ya tisini.

Wakati Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi akipitishwa na CCM kutetea kiti chake mwaka 1990, tayari habari za mageuzi zilikuwa zimetapakaa duniani na wakati huo Mwalimu Nyerere alishang’atuka Ikulu, lakini akaendelea kuwa mwenyekiti wa CCM.

Alitumia Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kueleza kilichokuwa kinaendelea, imani yake kwa siasa za chama kimoja na hasa kwa chama hicho, na umuhimu wa kuangalia suala la vyama vingi kwa kina kabla ya kulikubali bila tahadhari wakati litakapokuja.

Katika mkutano huo uliofanyika Agosti 16, 1990, Nyerere aliwaambia wajumbe kuwa mjadala wa mabadiliko ya kurejesha siasa za vyama vingi ulikuwa umeanza.

“Ndugu wajumbe, uchaguzi wa sasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge utaendeshwa kwa kufuata katiba yetu ya chama kimoja. Hatukusudii kubadili utaratibu huu kwa sasa,” alisema Nyerere katika hotuba yake iliyochapishwa katika kitabu cha “Wosia wa Mwalimu Nyerere kwa CCM” kilichotolewa na idara ya mawasiliano ya chama hicho 1991.

“Lakini mjadala juu ya utaratibu utakaoiongoza Tanzania katika siku za mbele umeshaanza na ni matumaini yangu kwamba utaendelea.”

Mwalimu Nyerere alieleza umuhimu wa kufuata katiba ya wakati huo ya chama kimoja na athari zake kisheria kwa anayeukiuka hadi hapo itakapobadilishwa.

“Lakini nchi hii inajitahidi kuwa nchi ya kidemokrasia ya chama kimoja na taratibu za mtu kutoa maoni juu ya mabadiliko au sheria iliyopo au ya katiba, wakati anafuata sheria zilizopo ni lazima uruhusiwe katika mfumo wowote unaoitwa wa kidemokrasia,” alisema Mwalimu.

“Kwa kweli sifa moja ya demokrasia ya kweli ni kwamba inawapa wachache nafasi ya kisheria ya kujaribu kushawishi wengi waone ubora wa maoni yao. Hii ndiyo njia pekee ya kuleta mawazo mapya na tabia mpya katika jamii kwa amani na utulivu. Ni demokrasia gani inayozuia wananchi kuihoji katiba yake au sheria nyingine yoyote ya nchi? Demokrasia ikichukua sura ya udikteta, udikteta wenyewe utakuwa na sura gani?”

Muasisi huyo wa Taifa la Tanzania alisema kwa wakati huo mjadala ulikuwa haujafikia hatua ya nchi kufanya maamuzi na hivyo wananchi hawakuwa wameujua uzito wa suala hilo.

“Maoni yangu binafsi ni kwamba si vizuri suala kubwa kama hili likaamuliwa kwa pupa. Ni vizuri tujipe muda wa kutosha kuelewa maana ya uamuzi wowote tutakaoufanya,” alisema Mwalimu Nyerere.

“Tukiamua kuendelea na chama kimoja, basi tuwe tumeelewa sababu zake na tukiamua kuanzisha mfumo wa vyama vingi, basi pia tuwe tumeelewa sababu zake. Kwa hiyo ni wajibu wetu kupima kwa makini sana hoja zinazotolewa na pande zote mbili za mjadala. Ndiyo maana ni vizuri mjadala upate muda wa kutosha na uendeshwe kwa makini.”

Alisema jambo kubwa kwa maendeleo ya nchi ni “kuendeleza demokrasia na si mfumo unaoiendesha” na kwamba suala hilo litakapoamualiwa na mkutano mkuu wa CCM, hoja zitakazotumika “ziwe na uhusiano na hali halisi ya mahitaji ya Tanzania kwa wakati huo”.

Hotuba ambayo ilipata umaarufu sana ni ile aliyoitoa kwenye mkutano mkuu wa CCM wa mwaka 1992 baada ya Tume ya Nyalali kuwasilisha ripoti ya maoni ya wananchi yaliyoonyesha kuwa asilimia 20 tu ndio walikuwa wakitaka vyama vingi.

Alitoa hotuba hiyo Februari 18, 1992 jijini Dar es Salaam.

“CCM si chombo kinachozama, ambacho baadhi ya watu waliomo wanataka kukimbia wasizame nacho. CCM ni chama chenye nguvu, na kama Tume ya Rais ilivyobainisha. Wananchi wengi wangependa tuendelee na utaratibu huu wa chama kimoja chini ya CCM,” alisema Nyerere.

“Ndiyo maana, mimi kwa upande wangu napenda mageuzi haya yafanyike hivi sasa. Maana kila mageuzi makubwa huhitaji kiongozi mwenye uwezo na anayeaminiwa na wananchi. CCM ni kiongozi mwenye uwezo huo na anaaminiwa na wananchi.”

Itaendelea kesho