Nyuki walivyoibua taharuki ajali ya basi, vifo vyafikia 15

Muktasari:
- Baadhi ya mashuhuda waliofika eneo la ajali iliyoua 15 mkoani Lindi, wamesema zoezi la uokoaji wa majeruhi lilikabaliwa na uwapo wa nyuki waliokuwa wanang’ata watu na kusababisha ucheleweshaji.
Lindi. Vifo vya ajali ya basi la Baraka Classic iliyotokea jana eneo la Mputa, Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi vimefikia 15 kutoka 14 huku mashuhuda wakieleza nyuki walivyochelewa uokoaji.
Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumatatu Novemba 27, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Makuri amesema dereva wa basi, Mshamu Omar alifariki akipatiwa matibabu hivyo kuongeza idadi ya vifo.
Amesema hadi jana mchana (Jumapili Novemba 26, 2023) vifo vilikuwa 14, ambapo abiria walikuwa 12 na watembea kwa miguu wawili pamoja na majeruhi 26 waliolazwa katika Hospitali ya Nyangao.
Kamanda Makuri amesema wataendelea kuujulisha umma juu ya hali za majeruhi na kuwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo kupunguza mwendokasi.
Mashuhuda waeleza nyuki walivyochelewa uokoaji
Baadhi ya mashuhuda waliofika eneo la tukio baada ya ajali hiyo wamesema zoezi la uokoaji wa majeruhi lilibaliwa na uwapo wa nyuki waliokuwa wanang’ata watu.
"Nyuki hao wapo siku zote ila baada ya kutokea ajali walianza kung'ata watu, tulilazimika kununua dawa ya kuulia wadudu pamoja na kuchoma matairi.
“Vifo vilivyotoķea pia vinaweza kuwa vimesababishwa na majeruhi kuchelewa kupata msaada,” amesema Juma Machalila shuhuda wa ajali hiyo.
Wakati huohuo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetuma salamu za rambirambi kufuatia vifo hivyo, huku kikitoa wito kwa polisi kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani na kuchukua hatua kwa wanaovunja sheria.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Paul Makonda ilieleza: “Chama cha Mapinduzi kinatoa salamu za rambirambi na pole kufuatia taarifa ya kuhuzunisha ya vifo 15 na m,ajeruhi 26, vilivyotokea Jumapili, Novemba 26, 2023 baada ya ajali ya gari la abiria, Kampuni ya Baraka Classic kukosa breki likiwa katika mwendo wa kasi.
“CCM inatoa wito kwa vyombo vinavyohusika kusimamia usalama wa raia na mali zao, zikiwemo sheria za usalama barabarani kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wanaokiuka taratibu.”imesema sehemu ya taarifa hiyo.