Olengurumwa ajitoa ubunge Ngorongoro, watatu wachukuwa fomu

Saturday October 23 2021
ccmpic

Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa

By Mussa Juma

Arusha. Wanachama watatu wa CCM wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha wamejitokeza kuchukuwa fomu za kuwania ubunge Jimbo la Ngorongoro kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Ole Nasha aliyefariki Septemba 27, jijini Dodoma.

Hata hivyo, Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa ametangaza kujiondoa katika mchakato wa kugombea ubunge.

Soma zaidi:CCM kuanza Leo kutoa fomu za ubunge Ngorongoro

Katibu wa CCM wilaya hiyo, Amos Shimba amewataja waliochukua fomu kuwa pamoja na Wakili Daudi Haraka, Mwenyekiti wa halmashauri ya Ngorongoro mstaafu Elias Ngorisa na Leyani Sabore.

Shimba amesema kesho Jumapili Oktoba 24 itakuwa mwisho wa kuchukuwa fomu na kurejesha.

"Tunaomba wajitokeza kuchukuwa fomu lakini wazingatie kanuni zetu ni marufuku kuanza kampeni ikiwepo kukusanya watu kabla ya wakati," amesema.

Advertisement

Shimba amesema Oktoba 25 itafanyika kura ya maoni ya wagombea ubunge Ngorongoro na majina yataanza kujadiliwa Oktoba 26 na wajumbe wa sekretarieti ya wilaya, Kamati ya maadili na Kamati ya siasa.

Olengurumwa ajitoa

Katika hatua nyingine Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa ametangaza kujiondoa katika mchakato wa kugombea ubunge.

Olengurumwa amesema licha ya kupokea maombi ya wakazi wa Ngorongoro kwenda kugombea lakini ametafakari suala hilo na kuona ni vyema kuendelea kusaidia jamii Kupitia kazi anayofanya.

"Nawashukuru sana kumuomba lakini najua Kuna wanaccm wengine ambao pia wanauwezo wa kuongoza Jimbo la Ngorongoro," amesema.

Amesema fomu za ubunge zitatolewa Kwa sh 100,000 kwa wanaccm ambao wanajua kusoma na kuandika wenye umri kuanzia miaka 18.

Wengine wanaotajwa kutaka kumrithi Ole Nasha ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Emanuel Ole Shangai na Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu (TOSCI). Patrick Ngwediagi.

Wengine ni Mratibu wa miradi katika shirika la baraza la wafugaji wanawake wa Ngorongoro (PWC), Alais Melau na mhadhiri chuo cha wanyamapori ya mweka, Dk Kakoi Melubo, Mkurugenzi wa shirika la.jamii ya wafugaji (TPCF), Joseph Parsambei.

Yumo pia Dk Elifuraha Laltaika, ambaye ni mhadhiri Mwandamizi wa sheria kutoka chuo Kikuu cha Tumaini Makumira ambaye aliwahi pia kuwa katibu wa hamasa wa UVCCM Ngorongoro na mjumbe Bodi mbalimbali za mashirika na shule.

Advertisement