Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pato la Mtanzania laongezeka hadi kufikia Sh2.88 milioni

Dar es Salaam. Tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa inayoishia mwaka 2025, inaonyesha wastani wa pato la Mtanzania kwa mwaka umeongezeka kutoka Sh322,597 mwaka 2000 hadi Sh2.88 milioni Desemba 2022.

Ongezeko hilo, linatajwa kuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa dira hiyo ya kwanza, inayotarajiwa kukoma miaka miwili ijayo na hivyo kufungua pazia la mchakato wa maandalizi ya dira mpya itakayoishia mwaka 2050.

Dira ya Taifa hutekelezwa kwa kipindi cha miaka 25 na iliyopo sasa ilianza mwaka 2000, wakati Tanzania ikiwa mikononi mwa hayati Benjamin Mkapa, aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu.

Ongezeko la pato hilo la Mtanzania lilidokezwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliposoma sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa dira ya Taifa ya mwaka 2025, mbele ya waandishi wa habari.

Alisema mwaka 2000 wastani wa pato la Mtanzania mmoja ulikuwa ni Sh322, 597 lakini sasa umeongezeka na kufikia Sh2.88 milioni.

“Sasa hapa kuna watu watasema mbona mimi sina hiyo Sh2.88 milioni, hesabu zinapatikana kwa kujumlisha mapato ya watu wote nchi nzima kisha yanagawanywa kwa idadi ya watu. Kwa hiyo huu ni wastani, wapo wenye zaidi ya kiasi hicho na wengine wana chini ya kiasi hicho,” alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, tathmini hiyo inaonyesha mafanikio katika kujitosheleza kwa chakula ambapo Tanzania imefikia asilimia 124 na lengo ni kufikia asilimia 140 mwaka 2025.

Mafanikio mengine kulingana na tathmini hiyo, ni kuongezeka kwa mtandao wa barabara za lami na zege na kupungua kwa vifo vya wajawazito.

Hata hivyo, alieleza mafanikio na changamoto za utekelezaji wa dira hiyo, yatasomwa siku ya uzinduzi wa tathmini ya dira hiyo itakayofanyika Desemba 9, mwaka huu mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia hali ya uchumi kuendana na uhalisia wa kipato cha Watanzania, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Laurence Mafuru alisema Serikali kwa sasa imejikita katika uchumi jumuishi.

Alisema ili kuwa na uchumi jumuishi Serikali inawekeza rasilimali katika sekta inayogusa Watanzania wengi kama ya kilimo.