Petroli, dizeli bei juu

Muktasari:

Watumiaji wa petroli, dizeli na mafuta ya taa wataendelea kuongeza fedha zaidi katika kila lita ya mafuta wanayonunua baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza ongezeko la bei Machi, 2021.

Dar es Salaam. Watumiaji wa petroli, dizeli na mafuta ya taa wataendelea kuongeza fedha zaidi katika kila lita ya mafuta wanayonunua baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza ongezeko la bei Machi, 2021.

Kwa miezi miwili mfululizo bei ya mafuta yaliyopokewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka huku sababu za mabadiliko hayo zikitajwa kuwa ni mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, Machi 2021 bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa Sh94, Sh82 na Sh94 kwa kila lita kwa mtiririko wa awali ikilinganishwa na ongezeko la Sh53, Sh134 na Sh119 lililokuwapo mwezi Februari.

Ikilinganishwa na mwezi uliopita, bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa sh93.77, Sh81.38 na Sh94.16 kwa lita katika mtiririko wa awali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo sasa wakazi wa Dar es Salaam watanunua petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa Sh1,981, Sh1,911 na Sh1,863 ikilinganishwa na Sh1,887, Sh1,829 na Sh1,769 ya Februari 2021.

Kwa mujibu wa Ewura pia wakazi wa mikoa ya Kaskazini yaani Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara watalazimika kuongeza fedha zaidi kila wanapohitaji huduma ikilinganisha na mwezi Februari.

Kwa wanunuzi wa rejareja wa petroli na dizeli kwa mikoa hiyo watalazimika kuongeza Sh163 na Sh85 kwa kila lita ya mafuta watakayonunua huku wanunuzi wa jumla wakilazimika kuongeza Sh162.12 na Sh84.80 kwa kila lita katika mtiririko wa awali.

Lakini kwa wanunuzi wa mafuta ya taa wataendelea kutumia bei zilezile zilizokuwapo mwezi uliopita.

Hiyo ikiwa na maana kuwa wakazi wa Arusha sasa watanunua petroli, dizeli kwa Sh2,139, Sh1,975 katika mtiririko wa awali  ikilinganishwa na Sh1,976 na Sh1,890 waliyokuwa wakinunua mwezi Februari.

Lakini mabadiliko haya ya bei hayajawagusa wakazi wa mikoa ya Kusini ambayo ni Mtwara, Lindi na Ruvuma kwa sababu Februari 2021 hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara.

Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Ewura.

 “Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.”

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja, adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” inaeleza taarifa hiyo.