PIC yatoa maagizo Wizara ya madini, Stamico

New Content Item (4)
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wakiwa kwenye moja ya chumba cha mitambo cha kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR).

Muktasari:

Kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) kilichojengwa na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kwa kushirikiana na Kampuni ya Lozera ya nchini Dubai kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za madini kwa siku kwa asilimia 99.9.

Mwanza. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa mitaji ya Umma (PIC) imeiagiza Wizara ya Madini na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuhakikisha migodi yote yenye ubia wa kuchimba dhahabu na Serikali inapeleka dhahabu inayochimba kusafishwa kwenye viwanda vya uchenjuaji vilivyojengwa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya kikao cha ndani na kamati hiyo leo Jumapili , Machi 26, 2023 iliyotembelea kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR), Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko amesema agizo hilo haliitaji mjadala litatekelezwa mara moja.

“Kamati imetupa maelekezo mblimbali ya kufanyia kazi; Wale watu wote walioajiriwa hapa ndani (kiwandani) tuhakikishe local content inazingatiwa, tunalifanyia kazi na tumeisha anza kulitekeleza,”amesema

 “Lamaana sana ni kutoa wito kwa watanzania wote, wachimbaji kwamba Serikali sasa imeamua madini yake yanayochimbwa ndani ya nchi yetu yaweze kusafishwa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi na huu ndiyo msukumo wetu mkubwa kwamba tumejenga hivi viwanda sio kwa kubahatisha, tumejenga hivi viwanda ili viweze kufanya kazi,”

Amesema wanakamilisha taratibu za kimataifa kuhakikisha madini yote ikiwemo dhahabu inayochimbwa nchini isafishwe ndipo iuzwe nje ya nchi.

“Tunakamilisha taratibu ambazo ni za kimataifa na zikikamilika hizo tutakuja na utaratibu ambao tutasema kabisa hakuna dhahabu ambayo haijasafishwa itasafirishwa nnje ya nchi kwa sababu sheria ya nchi imeeleza dhairi kwamba madini yote ambayo hayajaongezwa thamani hayatosafirishwa nje,”amesema Dk Biteko

Amesema Serikali imefanya kazi kubwa ya kupunguza kodi kwenye madini yanayouzwa nchini na anaamini mwaka huu wa fedha itakuja na kivutio kingine kwa ajili ya wachimbaji ili kuwavutia zaidi kupeleka madini yao kusafishwa kwenye viwanda vya uchenjuaji vilivyojengwa nchini.

Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kasulu Vijijini, Vuma Augustine ameipongeza Stamico kwa usimamizi mzuri wa kiwanda hicho na kuitaka kuendelee kubana matumizi na kufanya uwekezaji wenye tija ili kuzidi kutoa gawio serikalini. 

“Tumeona mradi mzuri, unatija, wa kisasa kabisa ambao una gharama ya zaidi ya Sh16 bilioni wenye lengo la kusafisha dhahabu na hatimaye kuepuka kusafirisha dhahabu ghafi,”

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amesema maelekezo ya kuhakikisha na wao wanapata faida kwenye kiwanda hicho kama wanavyopata wawekezaji kwa ajili ya faida yao, wizara na Taifa kwa ujumla watahakikisha wanayafanyia kazi.

“Tunapopata ugeni wa viongozi kama hawa wanaosimamia uwekezaji wa muhimili wa Bunge inakuwa ni faraja kwa sababu tunapata mawazo mapya, tunapata maelekezo na sisi tutayafanyia kazi, tutaongeza ufanisi na kiwanda hiki kitakuwa na manufaa makubwa sana,”amesema