Picha, video za ngono zinavyochangia kupunguza hamu ya tendo la ndoa

Muktasari:

  • Utandawazi na ongezeko la maarifa katika teknolojia ya vifaa ya mawasiliano umechangia kwa namna moja au nyingine kusambaa picha na video za ngono.

  

Dar es Salaam. Utandawazi na ongezeko la maarifa katika teknolojia ya vifaa ya mawasiliano umechangia kwa namna moja au nyingine kusambaa picha na video za ngono.

Picha na video hizo sasa zinapatikana katika kanda za video, simu za mkononi na kwenye kompyuta zenye mtandao wa intaneti kwa gharama nafuu na wakati mwingine zinapatikana bure.

Wataalamu wa afya na saikolojia wanaeleza uraibu wa video za ngono ni moja kati ya sababu zinazochangia kupungua kwa hamu ya tendo la ndoa, hasa kwa wanaume.

Akizungumza na gazeti hili, Mwanasaikolojia, Charles Muhando anaeleza uraibu wa video na picha za ngono husababisha upungufu wa hamu ya tendo la ndoa kwa namna mbili ambayo ni kwa mwanamume kukosa suluhisho la hisia zake baada ya kuangalia video au picha za utupu.

“Anapokosa suluhisho la hisia zake kwa haraka anaweza kujikuta anajichua na akiendelea na tabia hiyo huweza kujikuta katika uraibu wa kitendo hicho.

Pili alisema athari inayoweza kujitokeza ni kukosa hisia za kufanya tendo hadi atakapoangalia picha au video hizo.

“Pia anashindwa kudumu kufanya tendo la ndoa hadi aangalie picha au video za ngono,” aliongeza.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, Dk Shita Samwel anayeeleza kuwa kwa kawaida mwili umeumbwa kutamani tendo hilo kupitia binadamu, hivyo uraibu wa uangaliaji wa picha au video hizo husababisha akili pamoja na hisia kuhama kutoka kutamani tendo hilo kupitia binadamu kwenda kwenye picha ama video za ngono.

“Kiasili mwili umeumbwa kutamani tendo hilo kupitia mwanadamu na si picha wala video na tendo hilo huratibiwa na ubongo ambao hutoa maelekezo na amri, ili vichocheo vizalishwe mwilini kwa ajili ya kupata msisimko na hisia,” alisema na kuongeza ubongo una tabia ya kuhifadhi vitendo tunavyovifanya mara kwa mara na kuwa kama tabia.

“Hivyo mtu anapokuwa ameathirika na uraibu wa video hizo, kuna wakati huweza kutokea ili apate msisimuko au kuridhika katika tendo la ndoa inamlazimu kuangalia picha au video hizo.

“Wakati mwingine akirudi katika tendo la asili la kawaida mwili unakataa kwa sababu ubongo unakuwa umeshazoea kuamrisha hamu kupatikana kwa kupitia picha na video,” alisema.

Kauli hiyo inaendana na hali iliyomkuta kijana mmoja (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 28, anayeeleza kuwa amekuwa akijitahidi mara kadhaa kuacha tabia ya uangaliaji wa video hizo bila mafanikio.

Lakini, daktari wa binadamu, Dk Rachel Mwinuka anafafanua video za ngono husababisha uzalishaji wa homoni inayosababisha mtu kupata raha (Depomine) kwa wingi katika ubongo, hali inayompelekea sehemu husika kupata raha hivyo ubongo huathirika kutokana na wingi wa homoni hiyo, hivyo husababisha ubongo kubadili sehemu hiyo kwa kuipunguzia uwezo wa kutafsiri homoni hiyo.

“Hivyo ili mtu apate raha tena itambidi awe na kitu kitakachozalisha homoni hii kwa wingi, hapa ndipo mtu huzidisha kuangalia video za ngono kwa wingi tena tofauti tofauti.”

Aliongeza kuwa tatizo hilo huwapata watu wote, lakini waathirika wakubwa ni wanaume kutokana na kuwa na hisia zao zipo karibu zaidi ukilinganisha na mwanamke.

Dk Shitta aliongezea pamoja na uraibu wa picha na video za ngono, sababu nyingine zinazochangia tatizo hilo ni msongo wa mawazo, kuugua magonjwa sugu kwa muda mrefu, kupata ajali itakayoathiri maeneo ya uzazi pamoja na matatizo katika mfumo wa vichochezi.