Polisi Dar yadaka watatu wakidaiwa kuwa majambazi
Muktasari:
- Watu watatu wakamatwa kwa tuhuma za ujambazi na kumjeruhi mlinzi, watatu watoroka Jeshi la Polisi laendelea kuwasaka.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za ujambazi na kumshambulia mlinzi.
Usiku wa Novemba 16 mwaka huu, watu hao waliokuwa na wenzao wengine watatu wanadaiwa kuvamia eneo la kampuni ya Kijiji Park ambalo lipo Kibada, Kigamboni, Temeke linalomilikiwa na Jacob Brounschweiler raia wa Uswisi.
Taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro imeeleza kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kuvamia eneo la tukio wakiwa na silaha za jadi ikiwemo nondo na mapanga.
“Watuhumiwa hao walimfunga kamba mlinzi wa eneo hilo, wakamtishia kumuua kwa kumpiga na nondo kichwani...baada ya muda waliingiza gari aina ya Fuso tenki na kuanza kuiba mafuta ya dizeli na petroli yaliyokuwa kwenye matenki makubwa ya ardhini,” amesema Kamanda Muliro na kuongeza;
“Jeshi la Polisi baadae lilipata taarifa toka kwa watu wema na kufika haraka eneo la tukio. Mlinzi alikutwa akiwa kwenye hali mbaya, akaokolewa na baadae wahalifu hao walijaribu kuwashambulia askari ambao walijihami haraka na kuwajeruhi wawili miongoni mwao kwa risasi.”
Kamanda Muliro ameeleza kuwa watuhumiwa wawili waliojeruhiwa, walipelekwa hospitali wakiwa na hali mbaya na majina yao hayakuweza kufahamika.
Mtuhumiwa mwingine mwenzao aliyekamatwa eneo la tukio ni Nelson Mbewe (49) mkazi wa Ubungo Kibangu na anahojiwa kwa kina juu ya tuhuma hizo za unyang’anyi wa kutumia silaha kwa kuvamia eneo hilo.
Kamanda Muliro amebainisha kuwa wahalifu wengine wanaendelea kusakwa huku jeshi hilo likiwashukuru wananchi wema wanaotoa taarifa haraka zinazohusiana na uhalifu, ili jitihada za kuyazuia matukio kama hayo zifanywe zaidi kuliko mapambano.