Polisi Lindi kuwabana madereva

Muktasari:
- Jeshi la Polisi, kitengo cha Usalama Barabarani mkoani Lindi, kimebaini baadhi ya magari kuwa na hitilafu na kupakia abiria kupita kiasi, kuendesha kwa mwendo kasi jambo linaloweza kusababisha ajali.
Lindi. Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani hapa, limesitisha safari kwa baadhi ya magari ya abiria baada ya kubainika kuwa na hitilafu.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Desemba 12, 2023 na Mkuu wa kitengo hicho, Aimidiwe Msangi alipokuwa akifanya ukaguzi wa magari hayo, katika eneo la Sido lililopo Manispaa ya Lindi.
Kwa mujibu wa Kamnada Msangi, pamoja na kufanya ukaguzi jeshi hilo pia linatoa elimu kwa abiria kutokana na baadhi ya madereva kutokuwa makini hasa kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka, ambapo hawafuati sheria za usalama barabarani.
“Tumebaini madereva wengi hawafuati sheria za usalama barabarani huku wakipakia abiria zaidi ya kiwango walichopangiwa. Pia baadhi ya magari ni mabovu.
"Kuna gari mbili nimezisimamisha zisiendelee na safari yake hadi pale watakaporekebisha ‘shock up’ ambazo zimeharibika. Akishatengeneza, ataleta likaguliwe ndipo aendelee na safari. Pia kuna gari ilijaza zaidi ya abiria 10, nimemwambia dereva awashushe na awatafutie usafiri mwingine," amesema Msangi.
Nae, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Lindi, Hamisi Livembe amewataka abiria kutoa taarifa endapo dereva anaendesha gari katika mwendo wa kasi.
"Kipindi hiki cha likizo madereva wamekuwa wazembe sana, kwanza wanajaza kupita kiasi, tumeshatoa elimu kwa abiria na watakapoona kuna kasoro yoyote kwa dereva iwe mwendokasi, kutaka kupita gari lingine bila kuchukua tahadhari, wapige simu," amesema Livembe.
Hata hivyo, dereva wa basi ambalo limegundulika kuwa na linahitilafu, Jumanne Mohamed amekiri gari yake kuwa na tatizo na kwamba anakwenda kutengeneza na itakapokaa sawa atairudisha tena kwenye ukaguzi na wakishajiridhisha, wataendelea na safari yao.