Polisi waliochukua Sh73 milioni za msaidizi wa Mwalimu Nyerere jela miaka 20

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imewahukumu waliokuwa askari polisi watatu kifungo cha miaka 20 jela,  kwa kosa la kutumia vibaya madaraka yao na kumfanyia upekuzi haramu, Profesa Justin Maeda.
  • Profesa Maeda,  ni mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa Rais wa awamu ya kwanza Nyerere, akimsaidia katika masuala ya uchumi.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imewahukumu waliokuwa askari polisi watatu kifungo cha miaka 20 jela,  kwa kosa la kutumia vibaya madaraka yao na kumfanyia upekuzi haramu, Profesa Justin Maeda.

Profesa Maeda,  ni mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa Rais wa awamu ya kwanza Nyerere, akimsaidia katika masuala ya uchumi.

Askari hao walienda nyumbani kwake jijini hapa na kumbambikia kosa la kumiliki meno ya tembo na kuchukua Sh70 milioni kutoka kwake.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana baada ya hukumu kutolewa, Profesa Maeda amesema anachohitaji ni kurejeshewa fedha zake zaidi ya Sh70 milioni, akieleza kushangazwa na hukumu ya kuwafunga jela bila kuzungumzia juu ya fedha zake.

Ingawa Profesa Maeda ametaja Sh70 milioni, hati ya mashitaka ilitaja kiasi kilichochukuliwa kuwa ni Sh73 milioni.

"Nimeipata hii hukumu lakini mimi nilitaka warudishe fedha zangu. Sasa wamewafunga nitafuatilia Ofisi ya Mashitaka kujua hatua zaidi kwani hukumu haijazungumzia fedha zangu," amesema na kusisitiza ana imani suala la kurejeshewa fedha zake litafanyiwa kazi.

Ilidaiwa Machi 19, 2021, washitakiwa walienda nyumbani kwa Profesa Maeda na kufanya upekuzi kinyume cha sheria na kudai fedha hizo ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa tuhuma hizo walizodai ni nzito.

Shitaka lingine lilikuwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh73 milioni kati ya Sh100 milioni walizodaiwa kuomba. Kosa la tatu ni kusaidia kutenda kosa lililokuwa likimkabili raia pekee katika kesi hiyo, Wilfred Mollel.

Hukumu ilivyokuwa

Katika hukumu iliyotolewa juzi na Hakimu Mkazi, Regina Oyler, alisema shitaka la kuomba na kupokea rushwa na kosa la kusaidia kutenda kosa la jinai lililokuwa likimkabili Mollel pekee, halikuthibitika mahakamani.

Aliwaachia huru askari wanne pamoja na Mollel kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha shitaka kwa viwango vinavyokubalika kisheria.

Waliohukumiwa kifungo ni Mkaguzi wa Polisi, Hillary Komba na makonstebo (PC), Bartholomew Maya na Apolinary Bureta, ambao Mahakama iliwatia hatiani kwa makosa ya kutengeneza ili kumtisha Profesa Maeda awapatie fedha.

Kabla ya polisi hao kufikishwa katika mahakama ya kiraia, walishitakiwa katika mahakama ya kijeshi na kufukuzwa kazi na Jeshi la Polisi kutokana na utovu wa nidhamu.

Walioachiwa huru ni makonstebo Zakayo Mwamrima, Paulo Mgema na Obeid Ndauka, Inspekta Tito Korongo na raia pekee katika kesi, Mollel.

Hakimu alieleza kosa la kwanza lilikuwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh73 milioni, kosa la pili ni matumizi mabaya ya madaraka na la tatu lililomkabili Mollel ni kusaidia kutendeka kosa.

Hakimu Oyler alisema baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa mashahidi 13 wa upande wa Jamhuri na vielelezo saba, na utetezi wa washitakiwa, aliwaona watatu ndio wana hatia ya makosa hayo.

Alisema upande wa Jamhuri umethibitisha pasipo shaka kuwa washtakiwa hao watatu wana hatia ya kutumia vibaya madaraka yao kwa kufanya upekuzi nyumbani kwa Maeda pasipo kufuata sheria za nchi.

"Mahakama imewakuta na hatia na inawahukumu kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja baada ya kuthibitika kutenda kosa la pili kinyume cha kifungu cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa kitendo cha kufika nyumbani kwa Maeda na kufanya upekuzi pasipo kufuata sheria," alisema.

Tukio lilivyokuwa

Profesa Maeda akizungumza na Mwananchi Digital Machi 19, 2021 alidai polisi saba wakiwa katika magari mawili, wawili wakiwa na silaha walifika nyumbani kwake na kutaka kumfanyia upekuzi wakidai anamiliki meno ya tembo.

"Walikuja hapa nyumbani na kutaka kufanya upekuzi bila kiongozi yeyote wa mtaa au balozi na hawakutaka kupekua ndani ya nyumba au kwenye mabanda yangu ya kuku, walitaka twende shambani ambapo kuna mizinga ya nyuki," alidai Profesa.

Alidai wakiwa shambani walipekua mzinga mmojawapo na kudai kukuta vipande viwili ambavyo walisema ni meno ya tembo na walimweka chini ya ulinzi na kumpiga picha.

"Waliniambia hii kesi kubwa na wakinifikisha polisi haina dhamana kwani ni kesi ya uhujumu uchumi, hivyo waliomba niwape Sh200 milioni lakini baada kuwaambia sina na kuwaeleza fedha zilizopo benki walitaka Sh100 milioni," alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Maeda, alidai baada ya hapo walimpeleka polisi kituo cha Usa River na baada ya majadiliano yao, walitaka awakabidhi fedha ndipo mmoja wao aliongozana naye kwenye benki mbili na kuwakabidhi fedha taslimu Sh67 milioni.

"Kutokana na kutotimia Sh100 milioni nililazimika kuomba kwa ndugu zangu bila kuwaeleza shida yangu na nikawakabidhi," alidai Profesa Maeda katika mahojiano hayo.

Alidai baada ya kuwakabidhi, akiwa kituo cha Polisi Usa River walibadilisha maelezo na kuandika hawakukuta meno ya tembo, ndipo walipomwambia Sh50 milioni watazitumia kumaliza kesi na wao watagawana Sh20 milioni.

Kwa mujibu wa Profesa Maeda, katika mazungumzo hayo ndani ya kituo hicho, walimrudishia Sh30 milioni.

Katika miaka ya hivi karibuni, Jeshi la Polisi limejikuta katika wakati mgumu kutokana na baadhi ya askari wake wasio waadilifu, kujihusisha na vitendo vinavyokiuka mwenendo mwema wa jeshi hilo, vikiwamo vya jinai.

Februari mwaka jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alinukuliwa akisema katika kipindi cha miezi sita, jeshi hilo liliwafukuza kazi askari sita kwa utovu wa nidhamu na kufanya matendo yanayokiuka mwenendo mwema wa jeshi hilo.

Desemba mwaka jana, Jeshi la Polisi liliwafukuza kazi askari wawili wa kituo cha Mabatini jijini Dar es Salaam, waliodaiwa kumuua kwa kumpiga risasi mlinzi wa baa ya Boardroom, Riziki Azan, na mmoja tayari ameshitakiwa kwa mauaji.

Septemba 2021, Jeshi la Polisi liliwafukuza kazi askari saba wa kituo cha Ileje kwa kosa la kuvuka mpaka wa Tanzania na kuingia Malawi wakiwa wamevaa sare za jeshi hilo na silaha za moto, wakimfukuza bodaboda waliyemshuku kubeba mali za magendo.